Sunday, 11 August 2013

Wafanyakazi Mtibwa mahututi kwa kuumizwa na mashine

mse_sugar
Wafanyakazi watatu wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa wilayani Mvomero mkoani Morogoro wamelazwa katika hospitali ya Bwagala baada ya kuumia wakati wakifanya matengenezo ya moja ya mashine ya kusaga sukari na hali zao ni mbaya.Taarifa zilizotolewa na baadhi ya wafanyakazi wenzao ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini, walisema kuwa wafanyakazi hao, waliumia asubuhi baada ya mashine waliyokuwa wakitengeneza, mkanda wake kujiwasha na kuwajeruhi.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea tukio hilo na kuwataja watu hao kuwa ni fundi Salumu Hussein, Leon Batterzay ambaye anatarajia kuhamishiwa muhimbili jijini Dar es Salaam kutokana na hali kuwa mbaya pamoja na Maliki Kilimo ambaye pia yuko mahututi.

Shilogile alisema kuwa tukio hilo limetokea Agosti 5, majira ya saa 12 asubuhi kiwandani hapo baada ya mafundi hao kuwa katika matengenezo ya mashine hiyo.

Naye Meneja wa kiwanda hicho, Belnard Kiula alikiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa kwa suala kama hilo halikuwa na ulazima wa kuripotiwa polisi na badala yake taarifa zinatakiwa kuripotiwa Osha jijini Dar es Salaamu ndani ya masaa 24.
kwa hisani ya ASHTON BALAIGWA
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

0 maoni: