KIPA wa zamani wa Simba, Juma Kaseja amesema hajasaini mkataba wa kuichezea FC Lupopo ya DR Congo ila wapo kwenye hatua nzuri ya mazungumzo lakini akasisitiza kuwa bado ana mapenzi na klabu yake ya zamani ya Simba. Kaseja ameondoka kwenye kikosi cha Simba hivi karibuni baada ya uongozi kukataa kumuongezea mkataba ambapo kwa sasa Lupopo imekuwa ikifanya mazungumzo ya kumsajili, na ili kujiweka fiti, jana alitua kwenye mazoezi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Ustawi jijini Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaseja alisema mapenzi yake kwenye Klabu ya Simba yataendelea na kusisitiza kuwa kilichomuondoa ni kutofautiana na baadhi ya viongozi lakini hana chuki na Simba.
“Nimeondoka Simba sijagombana na mtu yeyote, bado naipenda kama klabu yangu ya zamani lakini kuna baadhi ya viongozi ndiyo waliosababisha mambo haya kutokea.
“Lupopo bado sijasaini ila tupo kwenye mazungumzo na tumefikia hatua nzuri tu, hapa Mtibwa nafanya nao mazoezi kwa kuwa ni marafiki zangu tu,” alisema Kaseja.
Aidha, taarifa ambazo gazeti hili lilizipata muda mfupi kabla ya kuingia mitamboni ni kuwa Kaseja atasaini mkataba wa kuichezea Lupopo muda wowote kwa kuwa alikuwa kwenye hatua za mwisho za kuafikiana kuhusu maslahi.
Kwa hisani ya Lucy Mgina na Martha Mboma/GPL
0 maoni:
Post a Comment