KIJANA mmoja, Twaha Ally (36 - pichani) ambaye alikuwa kondakta wa daladala linalofanya safari zake kati ya Majohe nje kidogo mwa Jiji la Dar es Salaam na Gongo la Mboto ameuawa mwishoni mwa wiki iliyopita na watu wasiojulikana waliomvamia na kumnyang’anya fedha. Marehemu alikutwa na mauti hayo baada ya kushambuliwa na watu hao kituo cha daladala baada ya kugoma kutoa fedha ambazo walitaka awepe.
Taarifa kutoka eneo la tukio Gongo la Mboto, zinasema kuwa Twaha baada ya kufika kituoni hapo alishuka kwa lengo la kwenda kununua sigara lakini alishitukia anazingirwa na watu asiyowajua wakimtaka awape fedha.
Aidha, inadaiwa wakati wa purukushani ya kumnyang’anya fedha, wapita njia walidhani ni watu waliotaniana lakini walishituka baada ya kijana huyo kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Shuhuda mmoja ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini alimueleza mwandishi wetu kuwa mara baada ya Twaha kuchomwa mwilini na vitu vyenye ncha kali, dereva wa basi alilokuwa akifanyia kazi alimpigia simu jirani yake na kumfahamisha kuhusu tukio hilo kushambuliwa.
Kwa kuwa Twaha alikuwa amefariki, alimfahamisha jirani huyo asiwaambie ndugu zake kwani angewachanganya. Hadi sasa haijajulikana marehemu alinyang’anywa kiasi gani cha fedha. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Marietha Minangi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu 28 walikamatwa, watatu wanadaiwa kuhusika na tukio hilo.
Kamanda huyo alisema msako huo ulifanywa kwa kushirikiana na polisi jamii na uongozi wa serikali ya mtaa huo na kuongeza kuwa zoezi hilo la kusaka wahalifu linaendelea.
Kwa hisani ya http://www.globalpublishers.info
0 maoni:
Post a Comment