RAHMA Al Kharusi si jina geni katika mchezo wa soka Tanzania, wengi wanamkumbuka wakati alipoamua kuingia katika kuisaidia Twiga Stars na baadaye akaipeleka nchini Marekani lakini baadaye akapotea. Akarejea akiwa upande wa African Lyon, akasaidia mambo mengi na kufanya timu hiyo izidi kupata umaarufu, lakini baadaye hakuonekana hadi alipokuja kuibukia Simba na kusema hapo ndiyo nyumbani.
Mfanyabiashara huyo bilionea anasisitiza ametua Simba baada ya kuombwa kukubali uteuzi wa mjumbe wa kamati ya utendaji na anaamini atakuwa mshindani mkubwa wa kuleta maendeleo.
Rahma ni Rais wa Makampuni ya RBP Oil ambayo yanafanya biashara mbalimbali katika nchi tofauti za Afrika. Baadhi ya biashara hizo ni uuzaji wa mafuta ya ‘dizeli’ na petrol katika nchi mbalimbali, lakini pia vyakula pamoja na samani za ndani.
Nchi za Afrika ambazo makampuni yake yanafanya kazi ni pamoja na Tanzania, DR Congo, Sudan Kusini na Uganda lakini pia kampuni zake zinafanya biashara katika nchi za Oman na Qatar.
Rahma, maarufu kama Queen of Bees, yaani Malkia wa Nyuki, anataka Simba yenye mabadiliko makubwa huku akitumia msemo wa, “Nikianza jambo, lazima nilimalize.”Anataka kuiona Simba ikiwa na mambo mengi yenye mabadiliko, lakini anataka timu ya wanawake pamoja na timu imara ya vijana ambayo itaiwezesha Simba kuwa na msingi hapo baadaye.
“Simba walikuja kuniomba, sikuona kama kuna ubaya wa kukubali kuingia. Wakati tunakua nyumbani nilikuwa nikimuona baba yangu akiisaidia Simba, nasi tukajikuta tunaingia Simba. Tangu nikiwa mdogo, hii ndiyo timu yangu.
“Huo ni ushabiki, lakini ninachotaka mimi ni maendeleo. Najua kuna presha kubwa kutoka kwa Yanga, mimi nitaichukulia kama changamoto na nitashindana kuleta maendeleo. Najua Yanga wanaye (Yusuf) Manji, nitashindana naye sana.
“Najua nikishindana na Manji nitaleta maendeleo upande wa Simba, lakini nitapenda uwe ushindani wa kimaendeleo na si zaidi. Kama nitaona ni ushindani wa kutaka kuumizana nitajiweka kando, nataka maendeleo ambayo ndiyo mafanikio.
“Sitaki ugomvi, ndiyo maana utaona nilijiondoa Twiga na African Lyon. Migogoro ni kati ya vitu nisivyopenda kabisa, halafu Manji ni mtu ninayeheshimiana naye sana. Hivyo sitaki malumbano ila ushindani wa kuleta maendeleo.
“Nitashirikiana na wenzangu kuifanyia Simba kila linalowezekana ambalo litaonekana ni kubwa. Safari ya hapa Oman nataka pia iwe ni yenye manufaa. Ndiyo maana niliwaambia wachezaji lazima wajitume na kuonyesha muda wao walioutumia hapa ulikuwa na manufaa.
Safari Oman: Ilikuwa Simba wapelekwe sehemu moja inaitwa Nizwa, ni kama kilomita 150 kutoka hapa Muscat, nikaona si sahihi. Natumia kama milioni 80 au zaidi kuihudumia Simba hapa maana wenyeji wao Fanja nao kama hawaihudumii vilivyo.
Sipendi wafike hapa halafu wateseke, ndiyo maana mambo yote ninayafanya kupitia RBP Group. Najua Simba inajiandaa na nina mpango wa kufanya mengi makubwa ikiwezekana.
Bima: Tayari tupo katika hatua za mwisho, ndani ya siku moja wachezaji wa Simba na viongozi watakatiwa bima ya maisha. Naamini ni kitu kizuri wakiwa na bima hasa hapa ugenini.
Najua fedha nyingi pia zitatumika lakini naona ni jambo la busara kufanya hivyo, maana sisi ni binadamu na hauwezi kujua kitakachotokea kesho.
Familia, kazi, Simba: Kweli ni kitu kigumu sana, lakini hayo tayari ni majukumu yangu. Ninapenda kufanya kazi kwa kujituma sana. Wakati mwingine nakesha nikifanya kazi hadi asubuhi maana nina ofisi nyingine Marekani, hivyo kuna vitu navifanya nikiwa hapa Oman au Tanzania, unajua tena dunia sasa ni kama kijiji.
Ugumu utakuwepo lakini sipendi kufeli katika lolote, ndiyo maana napenda kujituma ili nifanikishe kitu ambacho nimekianzisha au nimeingia na kuanza kukifanya.
Ubora: Ninaamini Simba ni timu bora, lakini lazima wajiandae vizuri na kufanya mambo kitaalamu. Kama watajaribu kubahatisha wataharibu kila kitu. Lakini kujituma pia ni msingi wa maendeleo, hivyo lazima kuwe na watu wenye nia ya kupata mafanikio.
Sisemi Simba itashinda kila siku, lakini ikipoteza basi lazima kuwe na hali ya kukubali, pia ni lazima watu wajitathmini kwa nini wamejikwaa. Mimi pia ninapenda kuona timu yangu inashinda kama ilivyo kwa mashabiki.
Malkia wa Nyuki: Hili jina nimebatizwa na watu kutokana na tabia yangu ya kupenda kufanya kazi kwa ushirikiano, lakini mara nyingi nimekuwa nikizungukwa na watu ambao wanapenda kuniona nipo salama.
Lakini kifamilia kuna jambo moja, karibu nyumba zangu zote, nyuki wamekuwa wakitengeneza mzinga. Hali hii imewashangaza ndugu na marafiki zangu wengi, hata mimi mwenyewe. Tayari nimelizoea hilo jina na ninaona kawaida ingawa sikulikusudia.
Rahma anaishi katika eneo la Al Kheri, moja ya vitongoji maarufu vya Jiji la Muscat, watu wengi wenye uwezo wa fedha wanaishi eneo hilo.
Nyumba yake inaweza kufikia thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.8, imejengwa kisasa huku ikiwa na mambo kadhaa ya kuvutia utafikiri zile nyumba za mastaa wa Hollywood au wanamuziki maarufu wa Marekani.
Ingawa kuna nyumba nyingi bora katika eneo hilo, bado yake inachomoza pekee na kuonekana moja ya nyumba bora kabisa.
Ukiingia getini, gari inapanda hadi juu ghorofa ya kwanza ambako ndiko kuna sebule, kila moja ikiwa imetengenezwa kwa mfumo wake. Ndani kuna sebule tatu huku kukiwa na vyumba zaidi ya vitano vya kulala.
Kuna vyumba viwili tofauti vya kulia chakula, kuna bwawa la kuogelea lililo ndani ambamo hakuna jua na AC zinawashwa ili kuleta kipupwe. Juu ya bwawa hilo kuna maporomoko ya maji ambayo yanaongozwa na umeme na kuna ukuta wa mawe ambao unafanya eneo hilo liwe kama ziwani.
Mbele ya bwawa hilo la kuogelea kuna ukumbi mdogo ambao bendi au kikundi cha taarabu cha watu kinaweza kutumbuiza na watazamani hadi 70 wakaingia na kuburudika kwa raha zao.
Ndani ya nyumba hiyo kuna ofisi kubwa ikiwa na chumba kidogo cha mikutano ambayo mara nyingi huitumia kufanya kazi zake kama anaamua kutotoka nje.
Kwa kuwa nyumba hiyo inajitosheleza kwa kila kitu, wakati mwingine Malkia huyo wa Nyuki, mama wa watoto pacha, hujikuta akiishi ndani ya nyumba hiyo hata mwezi mzima bila kutoka nje.
Picha zaidi za Malkia wa Nyuki hizi hapa
Kwa hisani ya GLP
0 maoni:
Post a Comment