Thursday 22 August 2013

Robert Mugabe kuiongoza Zimbabwe

Rais Mugabe
Robert Mugabe ameapishwa kwa mara ya saba kama kiongozi wa Zimbabwe. Siku hii ya Alhamisi imetangazwa kuwa siku kuu kuwawezesha wafuasi wa kiongozi huyu mwenye umri wa miaka 89 wahudhurie sherehe za kuapishwa. Sherehe za kuapishwa kwake zimekuwa zikicheleweshwa kwa sababu ya kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kupinga kuchaguliwa kwake na mpinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai , ambaye alidai kulikuwa na wizi wa kura.
Tsvangirai pia anadai wapiga kura wake milioni waliondolewa kwenye vituo vya kupigia kura katika maeneo ya mijini , yanayoaminiwa kuwa ngome yake ya kisiasa.
Itakuwa ni fursa nyingine kwa rais Robert Mugabe kutoa hotuba zake zenye makali hususan kuyashutumu mataifa ya magaribi kutokana na vikwazo vilivyowekewa zimbabwe na kuuponda upinzani unaoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Morgan Tsvangirai.
Ni nafuu kwa bwana Mugabe ambaye ilibidi agawane madaraka na Bwana Tsvangirai kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kufahamu kuwa mara hii atakuwa ni yeye pekee kwenye usukani wa kuiongoza zimbabwe.
Zaidi ya marais arobaini wa mataifa ya kigeni wamealikwa katika sherehe za leo lakini haijabainika ni wangapi watahudhuria kushuhudia kuapishwa kwa Robert Mugabe katika uwanja mkubwa zaidi wa michezo nchini Zimbabwe mjini Harare.
Leo Alhamisi imetangazwa kuwa siku ya alhamisi ili kuwaruhusu wafuasi wa rais huyo mkongwe kuhudhuria sherehe hizo.
Waandalizi wamesema kuwa sherehe za leo zinatarajiwa kuwa za hali ya juu kuliko sherehe za mwaka 1980 baada ya Zimbabwe kunyakuwa uhuru.
Hatua hii inalenga kuwashawishi raia kwamba uchaguzi uliofanyika ulikuwa wa haki baada ya shutuma kwamba kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura.
Mpinzani mkuu wa Bwana Mugabe Morgan Tsvangirai alipuuzilia mbali uchaguzi huo, akiutaja kuwa bandia na ambao haukuashirii matakwa ya watu wa Zimbabwe. Bwana Tsvangirai ametaka kufanyiwa ukaguzi daftari la kudumu la wapiga kura.
Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe ilitangaza kuwa chama cha Zanu PF kilishinda thuluthi tatu ya idadi ya viti bungeni na kwamba Mugabe alinyakuwa ushindi wa zaidi ya asilimia sitini ya kura zilizopigwa. Chama cha MDC chake Morgan Changirai hakikuhudhuria sherehe.

Kwa hisani ya BBC Swahili

0 maoni: