Thursday 23 January 2014

Mwinjilisti aua mke, ajinyoga

MKAZI wa Kijiji cha Gama, wilayani Bagamoyo, Elikia Daniel (35), ambaye pia ni Mwinjilisti wa Kanisa la Anglikan katika kijiji hicho, amekutwa amejinyonga baada ya kufanya ukatili wa kumuua mke wake, kwa kumkata panga kichwani. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa ukatili huo ulitoka Januari 20, mwaka huu, saa 10 jioni, wakati wapenzi hao wakiwa katika shughuli za kukata miti ya kutengenezea tanuri la mkaa.

Alisema mwanamke huyo, Mboni Patrick (28), kabla ya tukio walikuwa pamoja wakifanya kazi ya kuandaa tanuri hilo, huku wakikata miti pamoja na kuchimba mchanga wa kufunikia.

Alisema wakati mwinjilisti huyo akiwa anapanga tanuri, alikuwa na mtoto Sabina Gabriel (10), lakini wakati anajiandaa kufanya mauaji hayo, alimtuma nyumbani akaandae chakula cha jioni.

Alisema wakati mtoto huyo anarudi kazini, alibaini kufanyika mauaji baada ya kuona damu na mkono wa mama yake uliojitokeza katikati ya magogo kwenye tanuri ambao alikuwa ameufukia.

"Mwanamume baada ya kumkata panga mke wake katika upande wa kulia wa kichwa, aliamua kumchukua marehemu huyo na kisha kumfunika katika magogo ya tanuri walilokuwa wakiandaa, lakini mtoto alipofika aliona damu nyingi na mkono wa mama yake ukijitokeza, ndipo alipokimbia na kutoa taarifa," alisema Kamanda Matei.

Kamanda huyo aliongeza kuwa mwanamume baada ya kufanya kitendo hicho, aliamua kukimbia umbali wa mita 300, kisha kuchukua uamuzi wa kujinyonga.


Kwa hisani ya Mtanzania

0 maoni: