Monday, 6 January 2014

Mahakama yamfilisi WEMA

YAMETIMIA! Ni kweli hakuna marefu yasiyokuwa na ncha! Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu aliyesifika kwa kumwaga fedha kila kukicha  ameanza  kufilisiwa, Ijumaa Wikienda lina habari ya kipekee kuhusu mrembo huyo.


MAHAKAMA YAANZA
Achilia mbali watu binafsi wanaochukua vyao baada ya mambo kuzidi kumwendea ndivyo sivyo, habari ya uhakika ni kwamba Mahakama ya Ilala, Dar imeridhia kukamatwa kwa lile gari lake la kifahari aina ya Audi Q-7 lenye namba za usajili T 973 BUJ lililokuwa likiwakosesha akina dada usingizi na kukabidhiwa kwa mmiliki halali kwa kuwa Wema alikuwa nalo kimagumashi.
Gari aina ya Audi Q-7 lenye namba za usajili T 973 BUJ alilokuwa akiendesha Wema.


Kwa mujibu wa vyanzo vilivyoenda shule vya Ijumaa Wikienda, gari hilo lilikamatwa Januari 2, mwaka huu Namanga, Oysterbay jijini Dar likiwa mikononi mwa kijana wa kiume aliyedaiwa kuwa ni mdogo wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’.
“Alikuwa nalo yule dogo ‘waiti’, mdogo wake huyu msanii Diamond. Alikuwa na wenzake pale Namanga kuna kibarabara cha vumbi, walikuwa wanarekodi video. Jamaa walikuwa wanalifuatilia so lilipopaki ndipo wakalipiga ‘tanchi’ (kulikamata),” kilisema chanzo chetu cha kuaminika.
Gari hilo baada ya kukamatwa.
Ilifahamika kuwa gari hilo lilikamatwa na kampuni kiboko ya madalali wa mahakama nchini (court brokers) ya jijini Dar iitwayo Unyangala Auction Mart Ltd & Court Brokers yenye ofisi zake kwenye Jengo la Harbour View Tower ‘JM-Mall’, Dar.
WEMA ACHANGANYIKIWA
Habari za uhakika zilidai kuwa kabla ya kulipeleka ‘yadi’ dogo huyo aliyekamatwa na gari hilo aliwasiliana na Wema na kumjulisha ambapo ilisemekana kwamba bidada huyo alichanganyikiwa.
Baada ya pale walilipeleka gari hilo kwenye yadi yao hiyo kisha kuwasiliana na mmiliki halali tayari kwa kumkabidhi.

Gari hilo likikabidhiwa kwa mmiliki halali.
KWA NINI?
Habari za uhakika ziko hivi; Januari 17, 2013, mwanaume aitwaye Clement  (yule kigogo mume wa mtu aliyekuwa mpenzi wa Wema) aliingia kwenye makubaliano ya kulinunua gari hilo kutoka kwa jamaa aliyetajwa kwa jina la George Tesha.

ILIKUWAJE?
Habari zilizochimbuliwa zilieleza kuwa, Clement ana rafiki yake ambaye ana kidosho anayesukuma gari la aina hiyo jijini Dar es Salaam na ‘kuwatesa’ wanawake wenzake.

ETI WEMA AWE NG’ARING’ARI
“Clement naye akasema anataka baby wake (Wema) naye awe anawasumbua na ‘mkoko’ kama huo.
“Tatizo wakati ule magari ya aina ile yalikuwa yanahesabika mjini. Huku na huku Clement akaliona lile gari, akamfuata Tesha na kumbembeleza amuuzie ili akampe Wema naye awe ng’aring’ari mjini.

MAKUBALIANO YANAFANYWA, SHILINGI MILIONI 90
“Jamaa walikubaliana ‘dheni’ Clement akalichukua lile gari kwa makubaliano ya kulipa Sh. milioni 90 za Kibongo.

“Kuna ‘misteki’ aliifanya Tesha kwa kukubali kumpatia gari jamaa bila ‘keshi’ kwa sababu alimwambia amwachie ‘dheni’ akachukue cheki ya mkwanja kesho yake ofisini kwake maeneo ya Magogoni, Dar.
“Kilichotokea ni kwamba kila Tesha alipomfuata ofisini aliambiwa na walinzi kuwa hawezi kuonana na Clement na wakati mwingine aliambiwa hayupo.

NYUMBANI
“Tesha alifanya hivyo mara kwa mara huku miezi ikikatika. Ilifika wakati akaenda hadi nyumbani kwa Clement kule Masaki (Dar) lakini nako aliambiwa hayupo na kama vipi amfuate nyumbani kwa Wema, Kijitonyama.

“Tesha alikuwa hapajui kwa Wema hivyo alianza kupatafuta hadi akapapata nako aliambiwa jamaa huwa anafika na kuondoka zake.
KUMBE SIYO LA TESHA
“Wakati hayo yakiendelea, kumbe lile gari nalo halikuwa la Tesha. Lilikuwa la jamaa mmoja mfanyabiashara (haijulikani ni biashara gani) mwenye mkwanja wake aliyetajwa kwa jina la Shadrack Tweve.

MAHAKAMANI
“Tweve alipoona hivyo vihela (ilisemekana Sh. milioni 90 kwake haimnyimi usingizi) havipati ndipo alipoamua kwenda kufungua kesi ya madai katika Mahakama ya Ilala.

“Mahakama ikaendesha kesi Tweve akimdai Tesha gari lake huku Clement akitafutwa, maana alikuwa hapokei simu wala hajibu meseji zaidi ya kusikika tu mara leo kamfanyia Wema hiki, mara kesho kile.
“Kuna purukushani nyingi zilipita. Hatimaye mahakama ikaamua gari likamatwe akabidhiwe Tweve mzigo wake.

GARI LASAKWA
“Hata kabla ya hukumu ya kesi hiyo, jamaa walikuwa wakilisaka kwa udi na uvumba bila mafanikio.

LAONEKANA MEEDA
“Kuna siku lilionekana maeneo ya Meeda Bar (Sinza-Mori) lakini aliyekuwa nalo akalikimbiza kulificha nyumbani kwa mama Wema, Mariam Sepetu maeneo yaleyale.

LAFICHWA KWA MAMA DIAMOND
“Pia kuna siku nyingine lilionekana Kijitonyama lakini likakimbizwa kwenda kufichwa kwa mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ pale Sinza-Mori.
“Lakini sasa Wema hana tena lile gari na mmiliki halali ni Tweve,” kilitiririka chanzo chetu.

WIKIENDA MZIGONI
Baada ya kujikusanyia data hizo za kiuchunguzi, Ijumaa Wikienda lilifika kwenye ofisi za madalali hao lakini kabla ya kuonana na wahusika lilikutana na gari hilo likiwa ‘yadi’.

Mwanzoni makachero wetu walisita kwa kuwa namba na aina ya gari ni kweli ni lile la Wema lakini rangi ni ‘silva’ badala ya ‘dakibluu’.
KWA NINI ALILIBADILISHA RANGI?
Kuna madai kuwa, Wema alilibadilisha rangi ili lisikamatwe kirahisi kwa kuwa Clement alishaambiwa kuwa linasakwa.

Hata hivyo, walijiridhisha kuwa ni la Wema na kwamba alishalibadili rangi kwa ushahidi wa siku aliyofika nalo Mahakama ya Mwanzo, Kawe wakati wa msala wa Wema kumtandika makofi yule meneja wa hoteli.
Ijumaa Wikienda lilimvaa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Patrick Sanga ambapo alikiri kupewa kazi ya kulikamata gari hilo na kulikabidhi kwa Tweve.
KUMBE CLEMENT  ALIKIUKA MAKUBALIANO
“Huyo Clement alikiuka makubaliano hivyo mahakama iliamuru tulikamate hili gari na kulikabidhi kwa Tweve kwani ndiye mmiliki halali,” alisema Sanga.

Haukupita muda mrefu, Tweve na Tesha walifika ambapo walionesha kadi ‘orijino’ ya gari hilo (Global ina nakala) kisha gari hilo likakabidhiwa kwa Tweve.
AKABIDHIWA
Huku Ijumaa Wikienda likishuhudia, Tweve aliingia kwenye gari hilo, akaliwasha huku akilalamika kuwa limetumika mwaka mzima hivyo halifanani na lilivyokuwa awali.
“Anyway, bora nimelipata, tayari limetumika mwaka mzima so halipo kama mwanzo,” alisema Tweve.

UTEKAJI?
Wakati Tweve akitabasamu kwa kupata chake ndipo madai mengine mazito yakashushwa kuwa baada ya gari hilo kukamatwa Namanga likiwa na ndugu wa Diamond, Wema alikwenda Kituo cha Polisi Kijitonyama  ‘Mabatini’ kuripoti kuwa eti ametekwa na kuporwa gari hilo.

Ijumaa Wikienda lilichoma mafuta hadi Polisi Mabatini na kunusa dodoso zozote juu ya kuwepo kwa shitaka hilo ambapo ilibainika kuwa halipo na badala yake ikaelezwa kuwa inawezekana alikimbilia Kituo cha Polisi Oysterbay lakini huko nako halikuonekana shitaka hilo.
Baada ya kupata ishu hiyo, gazeti hili lilimtafuta Wema ambaye anadaiwa kumpiga kibuti Clement lakini akawa hapokei simu.
Hata alipofuatwa nyumbani kwake, Kijitonyama (Makumbusho) ilielezwa kuwa, Madam ambaye kwa sasa anaminya kimalavu na Diamond hayupo. Ijumaa Wikienda lilikwenda hadi ofisini kwake, Mwananyamala ambako palikuwa pamefungwa.
Kwa hisani ya GPL

0 maoni: