Monday, 28 October 2013

Malinzi rais mpya TFF

JAMAL Malinzi, jana alitangazwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kupata kura nyingi dhidi ya mpinzani wake, Athumani Nyamlani katika uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye Ukumbi wa Water Front jijini Dar es Salaam. Malinzi aliibuka kidedea baada ya kupata kura 73 huku Nyamlani akipata 52.

Uchaguzi huo ambao ndiyo mwisho wa utawala wa aliyekuwa rais wa TFF, Leodegar Tenga, ulianza majira ya asubuhi na kumalizika saa 8:30 usiku wa kuamkia leo. Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni, alisema kuwa kazi haikuwa ndogo na mchuano ulionekana kuwa mkali ingawa hakuna kura iliyoharibika hata moja. Mara baada ya kutangazwa kwa Malinzi, wajumbe waliokuwa kwenye mkutano huo walionekana kushangilia huku wengine wakienda kumkumbatia rais huyo mpya. Malinzi atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwenye shirikisho hilo kwa kuwa timu zote za taifa zimekuwa hazifanyi vizuri, lakini uendeshaji wa soka umekuwa wa kususua kwa kipindi kirefu.

Karia atwaa Makamu wa Rais, Madega chali
Wallace Karia ameibuka kuwa makamu wa rais baada ya kuwaangusha Ramadhani Nassib na Iman Madega ambao walikuwa wanawania wote nafasi hiyo. Awali, Karia ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, ameshinda baada ya kujinyakulia kura 67, Madega alijipatia kura sita huku Nassib akijipatia kura 52 kuonyesha kuwa mchuano ulikuwa mkali.

Wajumbe, Mosha apigwa chini
Davies Mosha ambaye alikuwa anagombea nafasi ya ujumbe wa Mkoa wa Kilimanjaro na Tanga, alijikuta akipigwa chini kwenye mikoa yote hiyo baada ya Khalid kuibuka mshindi kwenye kanda hiyo. Wajumbe waliofanikiwa kupeta na kanda zao kwenye mabano ni Wilfred Kidau (Dar es Salaam), Geofrey Nyange ‘Kaburu’ (Pwani, Morogoro), Khalid Mohammed (Tanga na Kilimanjaro), Kambi (Lindi, Mtwara) Msafiri Mgoyi (Tabora, Kigoma), Ayoub Nyenzi (Iringa), Mhagama (Ruvuma), Blassi Kiondo (Katavi, Rukwa).

Nyamlani atoroka ukumbini:
Majira ya saa tatu na nusu usiku, aliyekuwa mgombea wa urais, Athumani Nyamlani, alitoroka ndani ya ukumbi wa uchaguzi wakati kura zikihesabiwa na kuwaambia wapigapicha waliokuwa nje wampige picha. Nyamlani ambaye alikuwa anapambana vikali na Jamal Malinzi, alilakiwa na wapambe wake, lakini akawaambia kuwa wasiwe na wasiwasi kwani bado mambo ni mabichi ingawa picha ilionyesha kuwa ameshajua kuwa amepigwa chini. Baadhi ya wapambe wake walionekana kumpa pole huku mwenyewe akiwajibu kuwa wasiwe na wasiwasi. “Waandishi nipigeni picha lakini msiseme kuwa nimekimbia, natoka mara moja halafu nitarudi, huku ndani mambo bado,” alisema Nyamlani ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa makamu wa raia wa TFF, lakini hakurejea tena.

Malinzi asimamia kura zake mwenyewe
Malinzi, jana alisimamia mwenyewe kura zake wakati zikiwa zinahesabiwa. Wengine waliosimamia kuhesabu kura zao wenyewe ni Iman Madega na Wallace Karia ambao walikuwa wanagombea nafasi ya makamu wa rais.

Wapambe Simba, Yanga, washangilia pamoja
 Katika hali ambayo ilionyesha kuwashangaza wengi, mara baada ya taarifa za ndani kutoka kwenye chumba cha uchaguzi huo kutolewa nje kuwa Jamal Malinzi anaongoza, wapambe waliokuwa nje walishangilia pamoja bila kujali kuwa wao ni Simba au Yanga. Wapambe waliokuwa nje kuanzia asubuhi wakisubiri matokeo hayo wengine wakiwa wamevaa jezi za Simba, Yanga na Azam, walishangilia pamoja kuonyesha kuwa wote wanaukubali uongozi huo.

Rushwa
Mmoja wa mabaunsa na katibu wa mkoa mmoja, juzi usiku wanadaiwa walikamatwa wakiwa na kitita cha fedha jumla ya shilingi milioni 2.7, wakiwa pia na karatasi yenye majina ya wajumbe wa mkutano mkuu. Karatasi hiyo iliyokuwa na wajumbe hao, ilionyesha kuwa kuna majina ambayo yameshatikiwa kuonyesha kuwa wameshachukua mshiko wao. Wawili hao walikamatwa na kulazwa kwenye Kituo cha Polisi Kibangu na walitolewa jana mchana.


Kwa hisani ya GPL

0 maoni: