Leo nitazungumzia juu mbinu mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia katika kujijenga heshima katika jamii unayoishi. Kila mtu anapenda kutambulika na kuheshimiwa.  Sidhani kama yupo hata mtu mmoja anayependa kudharauliwa na kuonekana asiye na mpango katika jamii. Hiyo ndiyo imewafanya baadhi ya watu kufanya kadiri wawezavyo, kwa gharama yoyote kuhakikisha wanaheshimika.
Wapo wanaoamini kwamba heshima kwa binadamu hupatikana kwa kigezo cha umri, uwezo kifedha, elimu au sehemu anayoishi. Hiyo siyo kweli kabisa. Elewa kwamba unaweza kuwa na vigezo hivyo lakini bado ukawa huheshimiki katika jamii.


Wanasaikolojia wengi wamekuwa wakieleza kwamba heshima haiwezi kupatikana kwa njia ya mkato bali hupatikana kwa kuweka misingi imara ya muda mrefu. Ni vigumu sana kujijengea heshima kwa siku moja, wiki ama mwezi mmoja.
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kuzitumia kwenye kujijengea heshima katika jamii.

Unadhifu wako
Heshima siku zote huanzia kwenye vitu vidogo ambavyo unaweza kuvidharau lakini vina nafasi kubwa sana katika kukupa heshima mbele za watu. Mojawapo ni mavazi. Ni ukweli ulio wazi kwamba, mavazi ya mtu yanaweza kumshushia ama kumuongezea heshima mbele ya jamii.

Kwa mfano mbunge wa jimbo fulani anapoamua kuvaa suruali pana iliyoshuka mpaka kwenye makalio kama wafanyavyo vijana wa siku hizi ni wazi kwamba atakuwa amejishushia heshima mbele ya wale anaowaongoza.
Mwalimu anapoamua kuvaa kimini na kitopu kinachoacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake ni lazima wanafunzi, walimu 

wenzake na wazazi hawatamheshimu kwa sababu yeye mwenyewe ameshindwa kujiheshimu. Kumbuka kwamba kama unataka uheshimiwe anza kujiheshimu mwenyewe.

Inaelezwa kwamba mavazi yanachukua nafasi kubwa sana katika suala zima la kujijengea ama kubomoa heshima yako. Kwa maana hiyo basi unatakiwa kuwa makini sana na uvaaji wako kama kweli unataka watu wanaokuzunguka wakuheshimu.

Busara ya maneno
Uzungumzaji wako mbele za watu pia unaweza kukusaidia katika kukujengea heshima mbele ya jamii. Kusema ovyo na kutamka maneno machafu mbele ya watu huweza kukupunguzia heshima yako. Tambua kwamba, jinsi unavyozungumza inaweza kuwa rahisi kwa mtu kukutafsiri kuwa wewe ni mtu unayestahili kuheshimika ama kudharaulika. 
Unatakiwa kuwa makini sana katika kila neno unalolitamka.

Ukijaribu kuchunguza utabaini kuwa, wengi waliojijengea heshima katika jamii si waongeaji na hata wanapoongea huwa makini sana.

Unaweza kumkuta mtu anarudiarudia maneno au sentesi wakati wa kuongea, hafanyi hivyo kwa kuwa na tatizo la kigugumizi bali ni katika tu kuhakikisha anatoa neno sahihi na pale ambapo atagundua kwamba amekosea iwe rahisi kusahihisha.

Kwa hiyo unashauriwa kuwa makini katika kutamka maneno hasa mbele ya watu kwani huwezi kujua watu wanaokusikiliza wana ufahamu wa kiwango gani juu ya yale unayoyazungumza.

Tabia zako
Zipo tabia ambazo ukiwa nazo ni vigumu sana watu kukuheshimu hata kama utakuwa mtu mzima ama una fedha nyingi kiasi gani. Miongoni mwa tabia ambazo zinaweza kukufanya usiheshimike ni kujisikia, kiburi, dharau na majivuno.

Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa na tabia ambazo kila mtu atakupenda na kukupa heshima unayostahili. 

Kama wewe ni msomi, jitahidi sana kujiepusha na tabia ya dharau dhidi ya wale wasio na elimu kama yako kwa kuona kwamba hawawezi kukusaidia kwa lolote. Unapaswa kushirikiana nao katika kila jambo ndipo watakuheshimu na kukupenda.