MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji, ametangaza rasmi kutowania tena nafasi ya uenyekiti kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakaotangazwa baadaye mwakani. Manji alichukua wadhifa huo mwaka jana baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Lloyd Nchunga, aliyekuwa amebakiza miaka miwili ya uongozi wake klabuni hapo.
Manji ambaye pia ni mfadhili wa klabu hiyo alitoa tamko juu ya nia yake hiyo jana kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani, Kariakoo jijini Dar es Salaam huku akitoa sababu kuwa ni kuwapisha wengine wenye uwezo wa kuiongoza timu hiyo nao kuchukua jahazi.
Amesema ametangaza kutowania nafasi hiyo mapema ili kuwapa nafasi nzuri wanaotaka kufanya hivyo wajipange mapema.
“Sitagombea tena uenyekiti kwenye uchaguzi ujao, nitawaachia wengine waendeleze hapa nilipoishia mimi, nimetangaza mapema ili wanaoitaka hii nafasi wajipange, maana wapo wenye nia lakini wanahofia kuchuana na mimi.
“Ninaweza kugombea lakini si sasa labda baadaye na siyo uchaguzi huu, nitafikiria kwanza kabla ya maamuzi hayo,” alisema Manji.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa ataendelea kuiongoza Yanga kwa miezi saba iliyosalia.
Aidha, alisema kuwa bado tarehe rasmi ya uchaguzi huo haijafahamika na kudai kuwa itajulikana mara baada ya Mkutano Mkuu wa Yanga utakaofanyika Januari 19, mwakani.
“Nikishajitoa rasmi kwenye madaraka ya uongozi wa Yanga baada ya kuwa nimemaliza muda wangu nitaendelea kuwa shabiki wa kawaida wa Yanga kama ilivyo kwa wengine na kuhusu udhamini litabaki kuwa suala la klabu kuchagua mdhamini wao,” alisema Manji.
Kwa hisani ya GPL
0 maoni:
Post a Comment