Winnie Madikizela-Mandela, (77) aliinama kumbusu Graca Machel (68), kabla ya kukaa katika kiti cha tatu kutoka kile alichokalia mwanamke huyo. Graca Machel alimwambia maneno machache ‘dada yake’ Winnie wakati akimbusu. Wanawake hao wote wakiwa wamevalia majaketi meusi na vilemba, walikumbatiana kwa sekunde kadhaa huku Winnie akitabasamu na Graca akitazama mbele.
Wote wawili wanaheshimika nchini Afrika Kusini kutokana na sababu mbalimbali. Winnie anaheshimika kwa mchango wake mkubwa wa kupigania ubaguzi wa rangi; Graca kwa moyo wake wa kujitolea kumtunza kiongozi wao mpaka anafariki dunia.
Hata hivyo Winnie amekuwa akikosolewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ile ya kuruhusu wapinzani wake wauawe kwa kuchomwa moto wakitumia mafuta ya petroli na matairi ya magari.
Mwaka 1988 alipatikana na hati ya kumuua kijana wa miaka 14 ambaye ilidaiwa alimtuhumu kuwa kibaraka, hata hivyo hukumu yake ilipunguzwa kutoka kuwa kifungo cha miaka sita jela na kuwa faini.
Winnie pia anatuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake iliyodumu kwa miaka 38 ingawa 27 kati ya hiyo hakuwa na mumewe ambaye alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Robben.
Graca Machel alifunga ndoa na Mandela wakati wa sherehe yake ya kutimiza miaka 80. Pamoja na kuwa Winnie na Mandela walitengana, katika kipindi cha ugonjwa wake kilichodumu kwa siku 181, alikuwa akimtembelea mara kwa mara.
Mjane wa Mandela, Graca,ambaye pia ni mjane wa Rais wa zamani wa Msumbiji, Hayati Samora Machel, alitumia muda wote kuwa pembeni mwa kitanda cha Mandela mpaka alipokata roho.
Ndugu wa karibu wanasema, daktari aliposema hakuna kitu kinachoweza kufanyika kuokoa uhai wa Mandela, Winnie alifika nyumbani hapo na alikuwepo muda wote mpaka kiongozi huyo alipokata roho.
Tangu Mandela afariki, Winnie amekuwa akionekana sana tofauti na Graca. Jumapili ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku tatu tangu Mandela afariki, Winnie alikwenda kusali katika kanisa ambalo lilikuwa likifanya misa kuu ya kitaifa kumuombea Mandela .
Winnie alikaa pembeni ya Rais Jacob Zuma. Hata hivyo siku yake iliharibia na Mchungaji, Mosa Sono aliyekuwa akiongoza ibada hiyo baada ya kumtambulisha kwa jina la Graca. Kwa upande wake Graca alisali katika kanisa dogo lililopo karibu na nyumba ya Mandela.
Graca ni mdogo wangu
Kwa muda mrefu sasa Winnie amekuwa akisisitiza kuwa hakuna uhasama baina yake na Graca na anamuona kama mdogo wake kwa kuwa kiumri pia amemzidi.
Winnie aliwahi kunukuliwa akisema: “Namuita mdogo wangu, na yeye huwa ananiita dada, hata tunapozungumza huwa maongezi yanamuhusu mume wetu,” anasema Winnie.
Habari kwa hisai ya Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment