CHINA kumekucha! Sakata la kusafirisha madawa ya kulevya ‘unga’ linazidi kulitafuna taifa, safari hii limechukua sura mpya baada ya askari nchini China kufanya oparesheni maalum ya kuwanasa wahalifu wa biashara hiyo haramu nchini humo. Kwa mujibu wa chanzo makini kilichozungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu kutoka China, baada ya vyombo vya habari kuripoti mfululizo juu ya mfumuko wa biashara hiyo, askari waliandaa mpango maalum wa kuwanasa watu wanaojishughulisha nayo.
“Baada ya vyombo vya habari kuripoti sana juu ya kukithiri kwa biashara ya madawa kulevya, polisi wamecharuka na kufanya msako wa nguvu katika maeneo ambayo Watanzania na watu mbalimbali wa kutoka Afrika wanafikia hapa China,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina.
MSAKO WAANZA
Chanzo kilibainisha kuwa, Jumatatu iliyopita wiki hii walifanya msako huo katika mjengo maarufu kwa jina la Dragon polisi walivamia na kuwakuta Wabongo na raia wengine wa kigeni Wanigeria na Waghana.
WAKUTWA WAKIPIGA MSOSI
Habari zilieleza kuwa msako ulipoanza katika kila chumba cha ghorofa hilo la Dragon, watu hao walikutwa wakipiga msosi na kunywa pombe ambapo baada ya kuwaona askari hao walikurupuka.
Katika vyumba hivyo, polisi walisachi na kukuta pakti za madawa ya kulevya ambayo hayakuweza kufahamika mara moja ni aina gani sanjari na chupa za pombe kali.
“Watu zaidi ya 1,000 wamekutwa katika ‘ambushi’ hiyo ya polisi. Wanigeria ndiyo wengi zaidi, lakini pia kuna Watanzania 5 ambapo wawili kati yao inasemekana walikufa baada ya kutokea dirishani na kujirusha,” kilisema chanzo hicho.
KITANZI
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, wote walionaswa katika msako huo hakuna cha msalie mtume zaidi ya kunyongwa kwani sheria ya nchi hiyo ipo wazi wala hakuna kumulika tochi.
Alisema hata ikitokea kiongozi wa serikali amenaswa katika biashara hiyo, hakuna njia yoyote ya kumlinda zaidi ya kumnyonga mchana kweupe.
“Huku hakuna cha kiongozi wa serikali wala kibosile, mtu yeyote akikamatwa katika msala wa madawa ya kulevya kinachofuata katika maisha yake huwa ni kifo.
“Ndiyo maana hata wale walioamua kujirusha ghorofani waliona ni bora kufanya hivyo kwani hata wakifa ni sawa kuliko kukamatwa halafu kunyongwa,” kilieleza chanzo hicho.
BALOZI AITWA KUWATAMBUA WATANZANIA
Imeelezwa kuwa, baada ya polisi kuendesha msako huo, polisi waliwaita mabalozi wa nchi husika ikiwemo Tanzania kwa ajili ya kuwatambua raia wake.
“Ndiyo tunasubiri balozi wetu aende kuwatambua Watanzania, leo (Alhamisi) ameitwa. Lakini kuna tetesi kuwa miongoni mwa hao Wanzania watano, kuna mwanamke anaitwa Jack na mwingine anaitwa Walter,” kilisema chanzo hicho.
Kwa hisani ya Erick Evarist/GPL
0 maoni:
Post a Comment