Tuesday, 23 July 2013

Mafuta ya ubuyu yazua mapya

BAADHI ya wagonjwa wa Saratani waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road mjini Dar es Salaam, wamebainika wanatumia mafuta ya ubuyu wakati yanadaiwa kusababisha saratani ya ini. Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika taasisi hiyo, umebaini wagonjwa wengi wanatumia mafuta hayo kwa usiri mkubwa. Katika hatua nyingine, Chama cha Albino Tanzania (TAS), kimewataka watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaotumia mafuta hayo kuacha mara moja, hadi hapo Serikali itakapotoa taarifa rasmi kuhusu matumizi ya mafuta hayo kwa ngozi ya albino.

Katika uchunguzi huo, imebainika baadhi ya albino hutumia mafuta hayo kwa kujipaka huku wengine wakiwa na vidonda kwenye ngozi zao.

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Chama hicho Taifa, Ziyada Nsembo alisema, TAS hakina elimu kuhusu bidhaa hiyo, hivyo wanaotumia wanaweza kuathiri ngozi zao zaidi.

“Tunawataka albino wanaotumia mafuta haya waache mpaka Serikali itakapotoa tamko rasmi kuwa mafuta hayo hayana athari kwa ngozi ya albino.

“Ngozi ya albino ni nyepesi, ina uwezo mkubwa wa kupitisha kemikali ndani ya mwili, ikiwa hayafai kunywa basi kwetu hayafai hata kujipaka, maana wengine wana vidonda. 

“Tumeamua kutoa kauli hii kwa sababu kuna mafuta ambayo albino hatakiwi kupaka mchana, huwa hayana uwezo wa kukinga mionzi ya jua. 

“Haya mafuta ya ubuyu tunaelezwa kuwa yanalainisha ngozi, hatujui kama yanakinga ya mionzi ya jua, hilo ndilo tatizo letu, tunashauri yasitumike hadi wataalamu wa masuala ya ngozi ya albino watufahamishe,” alisema Katibu huyo.

Mmoja wa albino ambaye ni kiongozi, alisema ameshawahi kutumia mafuta hayo.

“Wapo albino wanaotumia haya mafuta, hata mimi ni mmoja wapo, ila sikujua kama yana madhara, kwa sasa nimeacha kutumia.”



Wagonjwa

Baadhi ya wagonjwa ambao wamehojiwa na gazeti hili (majina tunayo), wameeleza wameyatumia mafuta hayo kwa muda mrefu.

“Tangu nimeanza kutumia hakuna mabadiliko yoyote ambayo nimeyapata, ila kuhangaika tu, maumivu tunayoyapata ni makali sana, kwa hiyo akitokea mtu anasema dawa hii inaponyesha kansa tunatumia, ili kupata ahueni.

“Ndugu zangu, walikuwa wananiletea wodini, nimeyanywa sana na kupaka mwilini,” alisema mgonjwa huyo ambaye anatoka mkoani Singida.

Mgonjwa mwingine, anayetoka Mkoa wa Mwanza alisema: “Ikiwa mafuta haya yanasababisha saratani basi wagonjwa wengi wa saratani tutaendelea kufa kila siku, kweli tunayatumia.

Mmoja kati ya watu wanaowauguza ndugu zao, Joyce Mwakalinga alikiri kuwa baadhi ya wagonjwa wanatumia mafuta hayo, huku akieleza kuwa biashara ya unga wa ubuyu ndiyo imeshamiri zaidi wodini humo.

“Kuna mgonjwa amelazwa jirani na mama yangu, huwa namuona anakunywa mafuta ya ubuyu kila siku asubuhi na jioni, sijawahi kuona mafuta ya ubuyu yanauzwa wodini ila unga wa ubuyu ndio unauzwa sana. 

Mmiliki wa Kampuni ya MTOHA, inayozalisha mazao ya mmea wa mbuyu yakiwamo mafuta, mkoani Dodoma, Daudi Masudi alisema tangu Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), itangaze mafuta hayo si salama, soko la ndani limeporomoka kwa asilimia 80.

Hivi karibuni umeibuka mvutano kati ya wajasiriamali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ambapo wanadai kuwa mafuta hayo si salama kwa kunywa.

TFDA, inasema mafuta hayo yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya Cyclopropenoic fatty acids, ambayo huweza kusababisha athari ya kiafya endapo yatatumika kama chakula. 

Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula wa TFDA, Raymond Wigenge alisema TFDA imefanya tathimini ya kutosha ambayo imewalazimu kutoa tamko hilo.

“TFDA inatekeleza majukumu yake, hatuwahujumu wajasiriamali, madhara ya mafuta ya ubuyu tumeyaweka wazi mlaji anaweza kupata saratani ya ini.


habari na RACHEL MRISHO, DAR ES SALAAM / mtanzania

0 maoni: