Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amesema njia pekee ya kushinikiza serikali kuwasilisha muswada wa mabadiliko wa sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari ni vyombo hivyo kugoma nchi nzima. Amesema vyombo vya habari vimekuwa vikilalamikia kwa muda mrefu sheria hizo kandamizi kutofikishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa mabadiliko wakati wana uwezo wa kuungana na kugoma nchini na serikali ikapeleka muswaada huo bungeni.
“Nyinyi vyombo vya habari mna nguvu kubwa sana, kila siku mnalalamikia kwetu sisi wabunge kuhusu muswada wenu wa habari ambao unakaliwa na serikali kuwa haufiki bungeni, kwanini msiungane na kugoma nchi nzima tuone kama hautaletwa bungeni na serikali, tatizo mimi naona hamjaweka nguvu ya pamoja,” alisema Lema.
Lema alisema hayo wakati akichangia mada kuhusu changamoto zinazowakabili vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari katika kuripoti habari za Bunge iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).
Mbunge huyo alisema kuwa Wizara ya habari imekuwa ikishindwa kuwasilisha muswada huo wa kuondoa sheria kandamizi ili kutaka kuendelea kuvibana vyombo hivyo vya habari visiweze kuwa huru.
Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes, alivitaka vyombo vya habari kumpatia muswada huo yeye ili auwasilishe kama muswada binafsi katika Bunge.
“Mimi nilishasema siku nyingi, nipo tayari kushirikiana na nyinyi, nipeni muswada huo niufikishe bungeni, lakini mpaka leo sijapatiwa wakati kila siku mnaendelea kulalamika tu,” alisema Blandes.
Awali akiwasilisha mada, mwandishi mwandamizi, Deodatus Balile, alisema mchakato wa kuandika muswada huo ulianza mwaka 2007 na kuwasilisha kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, lakini hadi sasa serikali inaendelea kuukalia bila kuupeleka bungeni.
“Tuliandika miswada miwili na tukaikabidhi serikalini na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo wakati ule, George Mkuchika alikuwa akituonyesha katika mkoba wake kuwa sasa anaupeleka, lakini mpaka leo yupo Utawala bora, hakuna kitu ingawa na huo ulikuwa sehemu ya utawala bora, tunawaomba nyinyi wabunge mtusaidie,” alisema Balile.
Kwa hisani ya NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment