Ningependa kuona Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kinafutiliwa mbali kabisa kwani kimeshindwa kuondoa ama kupunguza matatizo yanayowakabili walimu. Chama hiki kimeshindwa kutetea maslahi ya walimu na kimeonyesha udhaifu mkubwa katika ufuatiliaji wa madai mbalimbali ya wanachama wake. Baadhi ya madai haya ni posho ya kufundishia ktk mazingira magumu, kupandishwa madaraja, malimbikizo ya posho mbalimbali na nyongeza ya mishahara.
Kwa jinsi hali inavyojionyesha, ni vigumu sana hiki chama cha sasa kuwatetea walimu ipasavyo. Wakuu wa CWT (Gratian Mukoba, Ezekiel Olucho na wengine) wanaofaidi matunda ya michango ya walimu katika chama, wameshindwa kabisa kuwasemea walimu dhidi ya ukandamizaji wa serikali wa muda mrefu. Kwanza nashangaa kwanini hawa viongozi wapo madarakani kwa muda mrefu hivi! Michango ya walimu kwa CWT imetumika kuwekeza vitega uchumi mbali mbali, kama vile Mwalimu House, ambapo matunda yake hayamnufaishi mwalimu isipokuwa mchwa wachache wanaojiita viongozi wa CWT.
Walimu hukatwa jumla ya mabilioni ya shilingi kila mwezi kutoka kwenye mishahara yao na pesa zote hizi hutumika kutunisha vitambi vya viongozi wa walimu huku walimu wakifa njaa bila sababu ya msingi. Wala matumizi ya michango ya uanachama hayajawahi kukaguliwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuona jinsi gani michango ya walimu inavyotumika na kama walimu wananufaika na pesa hizo au fedha inayotokana na uwekezaji wa fedha hizo. Ingekuwa jambo la msingi endapo michango hii ingewarejea walimu kupitia SACCOS au namna nyingine ambayo ingewanufaisha walimu kuliko kubunguliwa na bungu wachache kwa maslahi yao binafsi. Hatuwezi kuwa na chama kimoja kikubwa kabisa lakini ambacho hakina tija kwa wanachama wake.
Kwa kuwa chama hiki kimeshindwa kuleta tija kwa walimu, napendekeza kivunjwe kabisa na kusahaulika katika ardhi ya Tanzania. Chama hiki kivunjiliwe mbali ili kila mwalimu ashughulikie matatizo mwenyewe badala ya kuendelea kuwakamua walimu michango ya chama ambacho hakiwezi kuwatetea. Baada ya kuvunjwa, mali zake ziuzwe na pesa zitakazopatikana zigawanywe kwa walimu kulingana na muda wa mwalimu kazini na kiasi alichokuwa akichangia kwa mwezi.
Kufanya hivyo kutawapunguzia walimu wingi wa matatizo yanayowakabili kwani inaonekana kwamba hata chama chenyewe ni mzigo kwa walimu. Ndiyo. Kiasi cha michango kinachokatwa kutoka kwenye mishahara ya walimu kinatosha kabisa kupunguza umasikini wa kipato unaowakabili walimu endapo CWT itavunjwa na hivyo makato ya wanachama kusitishwa.
Lakini, kama nilivyodokeza hapo awali, adui wa walimu ni walimu wenyewe. Wengi wao wana uelewa mdogo wa mambo, hivyo CWT imekuwa ikitumia udhaifu huo kuwakandamiza walimu kwa muda mrefu sasa. Na serikali nayo, kwa upande mwingine, imekuwa ikitumia mwanya huo huo kugoma kuwaboreshea walimu mishahara, kuwapandisha madaraja au kuwalipa posho mbalimbali wanazostahili. Kwa mtaji huu, walimu watazidi kukandamizwa hadi pale watakapojitambua, kumjua adui yao wa kweli na kuchukua jitihada za kupambana naye hadi kumtokomeza.
Nategemea kwamba walimu mtaamuka kutoka usingizi wa pono mliolala na kuanza kushughulikia matatizo yenu kwa njia nyingine badala ya kuendelea kukitegemea Chama Cha Walimu ambacho kimeshindwa kushughulikia matatizo yenu ipasavyo. Inavyoelekea ni kwamba viongozi wa chama chenu ama wameamua kuwasaliti kwa kushirikiana na serikali kuwakandamiza au hawana uwezo wa kutosha kuikabili serikali iweze kuwatatulia matatizo lukuki yanayowakabili na ambayo yamekuwa yakichangia kushuka kwa ubora wa elimu. Na ni bahati mbaya kushuka kwa kiwango cha elimu hakiwaathiri watoto wa vigogo ambao husoma kwenye shule za binafsi zilizo walimu wa kutosha na bora, mazingira mazuri ya kujifunzia na vifaa kufundishia vya kutosha. Watoto wanaotabika katika shule hizi mbovu za serikali ni wale wa walalahoi ambao hata kula kwao ni kwa shida na taabu na ambao hawana uwezo wa kuwasomesha kwenye shule binafsi.
Mdau T
0 maoni:
Post a Comment