KWENU,
Wasanii wa kike Bongo. Ni imani yangu ni wazima wa afya njema na mnaendelea na pilika za hapa na pale ili mkono uweze kusogea kinywani. Ni jambo la kheri! Nimewakumbuka sana na nikatamani kuzungumza nanyi. Nataka kuwakumbusha sababu za ninyi kutokuwa na nafasi kubwa sana kwenye game. Mara kadhaa tumeona, msanii anawika na kipaji chake halafu baada ya muda anafifia.
Hapa nazungumzia sanaa zote Tanzania. Tukiangalia sanaa ya muziki upande wa Bongo Fleva (kwa mfano) utakuta wasanii ambao walitesa na kushika hatamu miaka ya 2000 wengi chali! Sogea hadi 2009, wengi wamepotea kwenye game. Nadhani aliyebaki na uhai katika kipindi hicho ni Lady Jaydee. Lakini ukiangalia kwa wasanii wa kiume ni tofauti. Wengi wanakwenda na kasi na wamedumu mpaka leo. Ngoja hapa nikutajie wachache tu; Ay, Inspekta Haroun, Profesa Jay, MwanaFA, Madee na wengineo bado wapo na wanafurukuta ingawa kuna kizazi cha sasa cha akina Diamond na wenzake. Hata kwenye uigizaji mambo ni yaleyale. Wasanii wa kike waliotamba na akina Richie, JB, Bishanga, Ray, Tino, Frank, Cloud, Checkbud, Dino, Mtitu, Rogers, Jengua hawapo kwenye sanaa tena. Wakati michezo ya kuigiza kwenye runinga ikitamba wakati huo (hasa miaka ya 2000 na kuendelea) makundi makubwa yaliyokuwa yakijulikana zaidi ni Nyota Ensemble ‘Mambo Hayo’, Kaole Sanaa Group, Chemchem Arts Promotion ‘Kidedea’ na Splendid Theatre Group. Ukweli ni kwamba wengi wa wasanii wa kike waliokuwa waking’aa kipindi hicho sasa hivi wamefifia au hawapo kabisa kwenye sanaa lakini kwa upande wa wanaume ni tofauti – bado wanatamba.
HALI ILIVYO
Kwa sasa wasanii wanaotesa ni wapya ambao wameingia kwenye filamu wakitokea kwenye sanaa nyingine kama urembo n.k lakini pia kuna wengine wapya walioibuka hivi karibuni ambao baadhi yao bado wanatesa. Wasanii wa zamani ama hawapo kabisa au wapo lakini wanacheza scene za kupita. Sinema nzima, msanii anaonekana scene tatu au nne.
TATIZO LIKO WAPI?
Kujisahau, kushindwa kudhibiti ubora, kukosa ubunifu na kwenda na kasi ilivyo ndiyo tatizo. Kwa mfano msanii aliyekuwa akicheza kama binti mrembo, mchumba wa mtu, miaka nane iliyopita, pamoja na kwamba ameshindwa kuhifadhi urembo wake bado anataka kucheza nafasi ileile! Kila siku wanazaliwa warembo wengine, soko linaangalia linamhitaji nani kwa muda husika. Ni vyema sasa kuwa wabunifu na kubadili aina za uchezaji na uhusika ili muendelee kuwa juu. Wasanii ambao ndiyo mmeingia kwenye sanaa hivi karibuni ni vyema mkajifunza kutoka kwa dada zenu. Hata kwenye muziki ni vilevile. Mwangalie Jaydee, pamoja na umri wake ameendelea kuutunza mwonekano wake, anakwenda na wakati na anajua mashabiki wanachotaka ndiyo maana mpaka sasa anang’aa.
UKWELI NI HUU
Yako malalamiko kwenye filamu kwamba (eti) watayarishaji wanawabania wasanii wa zamani na kuwaweka wapya (hasa warembo). Hili napingana nalo. Kikubwa ni ubunifu tu. Angalia ulipo na uhusika unaokufaa ili uendelee kubaki kileleni. Hata kama ndiyo umeanza, unaweza kuwa bora hata miaka 20 ijayo kama utajitunza. Ipo mifano mingi, Nigeria panatosha kuwa somo kwetu. Wasanii kama Omotola Jalade, Mercy Johnson, Nkiru Silvanos, Rita Dominic kwa miaka mingi wamekuwa waigizaji Nollywood, lakini wameendelea kutunza mionekano yao hadi sasa wanaonekana bado warembo na wanatesa kwenye sinema. Ukiachana na mengine yote, mtindo wa maisha, mazoezi na aina ya vyakula unachangia. Wasanii wetu hawana ulaji ulio sahihi. Kwao nyama choma, chips mayai na bia ndiyo mpango mzima. Baada ya miaka mitatu kweli utaendelea kubaki na mwonekano uleule kwa ulaji huo wakati hata mazoezi hufanyi?
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa
0 maoni:
Post a Comment