Tuesday, 24 September 2013

Samantha Lewthwaite: Gaidi anayedaiwa kuilipua Kenya

TAIFA la Kenya, limekumbwa na tukio ambalo haliwezi kusahaulika masikioni mwa watu ambao ni wapenda amani. Tunavyosema hivyo, tunaamini kila mmoja anaelewa vizuri tukio la watu wanaosadikiwa kuwa magaidi, ambao waliteka jengo la Westgate mjini Nairobi na kusababisha vifo vya watu 69, huku 175 wakijeruhiwa vibaya.
Lakini katika tukio hilo, kuna mwanamke mmoja raia wa Uingereza mama wa watoto watatu, anadaiwa kuwa ni mmoja wa magaidi walioshiriki katika tukio hilo.

Mwanamke huyo mwenye itikadi kali, Samantha Lewthwaite, anajulikana kama ‘Mzungu Mjane’, ni mwanachama muhimu wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu Al-Shabaab la nchini Somalia, ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.

Mwanamke huyo, ambaye amewahi kuwa askari wa Uingereza kutoka eneo la Aylesbury, Bucks, alisilimu dini kuwa Muislamu ambaye mumewe alikuwa mmoja wa watu waliojitoa mhanga wakati wa mashambulizi ya Julai 7,2005 mjini London.

Vyanzo vya habari, vilisema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29, huenda ni miongoni mwa wanamgambo hao walioficha sura zao ambao hadi tunaingia mitamboni jana jioni, walikuwa wamejichimbia katika kituo hicho cha biashara.

Picha za mitandao ya kijamii zilionyesha mwanamke huyo akiwa ameshikilia bunduki.

Katika ujumbe wa Twitter, kundi la Al-Shabaab lilimsifu mama huyo maarufu ‘Mzungu Mjane’ na lilijigamba kwamba liko pamoja nao.

Katika akaunti yao ambayo imekuwa ikifungwa mara kwa mara, waliandika: “Sherafiyah Lewthwaite aka Samantha ni mwanamke shupavu,tuna furaha kuwa naye!” 

Umwagaji damu huo umeua watu 69 na 175 wakiwa wamejeruhiwa vibaya,wakiwamo watoto wenye umri hadi miaka miwili. 

Ilianza saa 7 mchana Jumamosi, wakati wanamgambo wanaofikia 15 wakiwa na silaha nzito walipovamia jengo hilo la maduka ya kifahari lililopo kaskazini magharibi mwa Jiji la Nairobi na kurusha magruneti na risasi kiholela, huku wakiimba nyimbo za jihad.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Manoah Esipisu alithibitisha ripoti kuwa mwanamke mzungu alikuwa miongoni mwa wanamgambo hao. 

Chanzo cha habari cha polisi nchini Kenya kilisema: “Samantha Lewthwaite ni shabaha namba moja.”

Wakati maofisa wa usalama wakijiandaa kuanza shambulio la mwisho usiku wa kuamkia jana, katika jaribio la kuhitimisha umwagaji damu, maofisa wa Serikali walifichua kuwa wanamgambo hao walikuwa wakishikilia mateka takribani 30.

Chanzo kimoja kiandamizi kilisema: “Kuna uwezekano mkubwa Samantha Lewthwaite akawa mmoja wa magaidi. Tuna ripoti za kuwepo mwanamke mmoja au ikiwezekana wawili wanahusika na shambulio hili.”

Kiliongeza: “Kuna ishara kubwa, Lewthwaite ana uwezo na ushawishi ndani ya Al-Shabaab kuendesha unyama kama huo.”

Lewthwaite, ambaye mumewe mwenye itikadi kali ya Kiislamu, Jermaine Lindsay, alijilipua katika njia ya treni ya Piccadilly mjini London Julai 7, 2005, pia anasakwa kwa njama za ulipuaji bomu ambalo liliua mamia ya watalii wa Uingereza mjini Mombasa. 

Pamoja na Mwingereza mwenzake, Jermaine Grant wawili hao walikuwa wamebakiwa na siku chache tu waendeshe shambulio lao kabla ya kukamatwa Desemba, 2011.

Grant kutoka London Mashariki, alitarajia kupanda kizimbani mjini Mombasa jana. 

Alikamatwa kabla ya mpango wao hatari kufanikiwa, lakini Lewthwaite alifanikiwa kutoroka tangu hapo. 

Hivi karibuni aliandika katika blogu yake: “Hofu inaweza kukufanya ufanye vitu vingi.”

Lewthwaite pia amehusika kutoa mafunzo kwa washambuliaji wa kike wa kujitoa mhanga katika nchi jirani ya Somalia.

Ilikuwa safari ya kutisha kwa mwanamke huyo aliyezaliwa kama msichana wa kawaida huko Aylesbury, kabla ya kukutana na Lindsay, ambapo wawili hao walioana miaka mitatu baada ya kukutana.

Wakati mumewe alipotajwa kuwa mmoja wa watu wanane waliojitoa mhanga katika njia za ardhini na kuua watu 52 mwaka 2005, Lewthwaite awali alilaani shambulio lililofanywa na mumewe na alikana kuhusika au kujua mpango wa mumewe.

Kumbe huo uliokuwa uongo mtupu, kwani miaka minane baadaye, Lewthwaite akatokea kuwa mmoja wa watafutaji wakuu wa wapiganaji kwa ajili ya mtandao wa Al Qaeda kwa ukanda wa Afrika Mashariki na msemaji rasmi wa Al Shabaab.

Pamoja na kuyalenga mataifa ya magharibi, Lewthwaite aliwahi kutumia mtandao wa Twitter kulaani makundi mengine hasimu ya kigaidi.

Hasira zake dhidi ya makundi hayo, zilijionesha kwa kifo cha Omar Shafik Hammami, mwanafunzi wa zamani kutoka Alabama. Wiki iliyopita alipigwa risasi na kufa katika shambulio la kushtukiza na magaidi wanaomtii ‘Mzungu Mjane. ‘Kifo chake na kiwe fundisho kwa wale wanaotaka kufuata nyayo zake,’ Lewthwaite aliandika katika mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, hakueleza kuhusu mwanaume wa Uingereza anayeelezwa kuwa mumewe wa pili aliyeripotiwa katika shambulio hilo la kushtukiza nchini Somalia, baada ya kundi la Al-Shabaab kuingia mzozo wa uongozi.

Sifa yake ya kutoogopa kitu barani Afrika ambako mitandao ya kigaidi inazidi kukua, inaimarishwa na kuhusika kwake kama mujahid au shujaa, wakati wa mlolongo wa mashambulizi na ulipuaji mabomu katika maeneo ya kitalii.

Akijulikana na wafuasi wake kama Dada Mzungu, Lewthwaite alihamia Kenya akiwa na watoto wake watatu mwaka 2007.

Akiwa na umbo dogo na fupi, alikatisha uhusiano na familia yake nchini Uingereza na kuzamia kwenye mitandao ya kigaidi Afrika Mashariki, akiunganisha nguvu na Waingereza wenye itikadi kali ambao waliingia Kenya kuendesha vita ya ‘jihad’ dhidi ya wasio Waislamu. Ilikuwa mwaka jana maisha mapya ya siri ya Lewthwaite yakaibuka.

‘Mwanamke mzungu’, aliyetambulika kama Lewthwaite, aliongoza kundi la magaidi kurusha maguruneti katika baa mjini Mombasa, ukanda wa pwani wa kitalii maarufu kwa watalii wa Uingererza. 

Watu watatu, akiwamo mtoto waliouawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.

Haikuchukua muda akawa katika rada za maofisa wa usalama wa Kenya,lakini aliweza kuwakwepa kwa kuvalia mavazi ya Kiislamu akifunika uso na mwili mzima akitembelea kati ya Somalia, Kenya na Tanzania.

Kwa hisani ya Mtanzania
Picha - thesun

0 maoni: