AMEZALIWA maskini, ameishi kwenye umaskini, kukosa mahitaji muhimu, akakosa elimu na fursa mbalimbali za maendeleo lakini hatimaye kipaji cha kuigiza kinakuja kumtoa. Huyo ndiye Van Vicker (pichani kushoto). Staa huyo ambaye ana mvuto runingani, alikanyaga ardhi ya Jakaya Kikwete, Tanzania mwishoni mwa wiki iliyopita kwa shughuli za kikazi na Amani lilifanikiwa kufanya naye mahojiano:
KUZALIWA
Alizaliwa Agosti 1, 1977 nchini Ghana. Wazazi wake wana asili ya mataifa mawili tofauti. Baba yake ni raia wa Uholanzi, mama yake ni raia wa Ghana na Liberia. Staa huyo anasema alipozaliwa wazazi wake walimpa jina la Fhiphi. Neno hilo ni la Kighana, linamaanisha mtu aliyezaliwa Ijumaa. Jina la Van lililokuja baadaye pia ni neno la Kiholanzi ambalo maana yake ni ‘mtoto wa’. Vicker lilikuwa ndiyo jina la baba yake hivyo Van Vicker maana yake ni mtoto wa Vicker. Hata hivyo baadaye mkali huyo alibatizwa kanisani na kupewa jina Joseph. Baba na mama wa staa huyo walikutana Liberia ambapo baba yake alikuwa akifanya kazi kwenye shirika moja la ugavi wa umeme nchini humo.
PIGO
Akiwa na umri wa miaka sita, Van Vicker alipata pigo la kuondokewa na baba yake.“Siwezi kuzungumzia sana suala hilo yule ni mzazi wangu japokuwa sikubahatika kupata malezi yake, toka hapo maisha kwangu yalikuwa magumu,” alisema Vicker.
ELIMU
Mkali huyo hakutaka kuzungumzia sana elimu yake, lakini aliweka bayana kuwa ana maarifa ya kutosha na zaidi hupenda kujielimisha mwenyewe juu ya mambo mbalimbali ya kila siku. “Elewa tu kwamba nilisoma katika ngazi ya kawaida, nilipata bahati ya kusoma shule ambayo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alisoma. Inaitwa Mfantsipim,” alisema.
KABLA YA KUIGIZA
“Kabla sijaanza kuigiza, nilikuwa Mtangazaji wa Radio Groove 106.3 FM ya Ghana,” alisema Vicker na kuongeza: “Kabla sijaanza kutangaza, nilipitia msoto wa hali ya juu kwani wakati huo pia sikuwa na baba. Maisha yalikuwa magumu, kila mtu alinitenga, nilidharaulika sana, machozi yalikuwa sehemu ya maisha yangu.”
KUIGIZA RASMI
“Mwaka 1999 nilikutana na jamaa mmoja, akaniunganisha kwenye dili la filamu, nikacheza filamu kwanza iitwayo Devine Love, hapo ndipo maisha yalipoanza kuninyookea,” alisema.
MAPENZI VIPI?
“Sikuwahi kujihusisha sana na masuala ya mapenzi utotoni, kutokana na jinsi hali ya kutengwa. Nilianza kupigana na maisha baada ya kutoka shule,” alisema. Mwigizaji huyo alizidi kutiririka kuwa, alikutana na mkewe Adjoa mwaka 1999 wakadumu kwenye uhusiano wa kimapenzi na kufanikiwa kufunga ndoa mwaka 2004.
WATOTO
Kwa sasa Van na mkewe wana watoto watatu, J’dyl, J-ian na Joseph Van Vicker II (pichani). Anasema hana mpango wa kuongeza watoto.
MICHEZO ANAYOIPENDA:
Mbali ya uigizaji, Vicker anapenda sana michezo kama mpira wa miguu, tennis na basketball.
Kuhusu mafanikio, mwigizaji huyo hakutaka kufunguka moja kwa moja utajiri wake lakini alidai kipato anachokipata kutokana na sanaa kinamwezesha kufurahia maisha yake.
TUZO
Vicker aliweka wazi kuwa amewahi kushinda tuzo mbalimbali lakini ambazo hawezi kuzisahau ni mbili za mwanzoni ambazo ni Ghana Awards Best Actor (Local Films) na Ghana Award Best Director (Leading Role).
BAADHI YA KAZI ZAKE:
Vicker amefanya kazi nyingi sana za kuigiza, kwa harakaharaka alisema anakumbuka sinema kama mia moja, lakini anazozikubali zaidi ni Devine Love, In the Eyes of my Husband, River of Tears, Innocent Soul, American Boy na Beyonce: The President’s Daughter.
AMEJIFUNZA NINI TANZANIA?
“Kila mtu ni mpole, mkarimu, mcheshi hivyo vitu vikubwa ambavyo nimejifunza Tanzania,” alisema Vicker.
Habari kwa hisani ya GPl
0 maoni:
Post a Comment