Sunday, 29 September 2013

Amigolas: Nimefanya kazi Twanga miaka 18 bila mkataba

Mwanamuziki  mkongwe Hamis Kayumbu maarufu kama Amigolas,  aliyeitumikia  Bendi ya African Stars (Twanga Pepeta), amesema kuwa licha ya kudumu na bendi hiyo kwa miaka 18 hakuwahi kuwa na mkataba. Amigolas ambaye hivi karibuni amejitoa kwenye bendi hiyo alisema kuwa hata alipoondoka na kuamua kupumzika hakutoa taarifa kwa mtu yeyote kwa kuwa alikuwa huru kufanya hivyo.
Akizungumza na Starehe, Amigolas alisema ingawa hataki kuzungumzia zaidi suala hilo,  lakini hata mafao ya uzeeni alianza kuwekewa miaka miwili iliyopita.
“Sitaki kuzungumzia sana suala hilo kwa kuwa halina faida kwa sasa, lakini sikuwahi kuingia mkataba na Twanga licha ya kufanya kazi kwa miaka 18. Hii inaonyesha jinsi gani wasanii wa muziki wa dansi nchini walivyo na wakati mgumu. Kubwa kwangu kwa sasa ni kwamba, naenda kuanza maisha mapya,” anasema Amigolas.
Amigolas anasema wanamuziki wa muziki huo wanapata wakati mgumu katika utendaji wao wa kazi kwa kuwa wadau wa muziki wamesahau muziki wa dansi na kuhamia kwenye Bongo Fleva.
Mwanamuziki huyo ambaye alikuwa ni mfano wa kuigwa kwa wanamuziki wa muziki wa dansi kwa kudumu kwenye bendi moja kwa muda mrefu, alisema hana kinyongo na mmiliki wa African Stars, Asha Baraka licha ya kukatishwa tamaa na mfumo wa uendeshaji wa bendi hapa nchini.
“Siwezi kujinadi kuwa muziki umenifanyia hiki umenifanyia kile zaidi ya kuwa maarufu na kujuana na watu,” anasema Amigolas.
Hata hivyo, Asha Baraka mwenyewe haonekani kuguswa  na kuondoka kwa wasanii wake katika bendi hiyo, huku kumbukumbu zikionyesha kwamba mbali na Amigolas wengine waliohama kutoka African Stars  ni Msafiri Diof, Rogat Hega ‘Katapila’ na Victor Mkambi.
“Mimi sina tatizo na kuhama kwa Amigolas, kwani nimekuwa naye kwa muda mrefu, sasa umri wake umeshakua mkubwa na hawezi tena mikiki mikiki ya muziki wa kileo. Zamani aliweza kuimba kuanzia Jumatatu hadi Jumatatu, lakini kwa kipindi kirefu sasa anaimba mara moja kwa wiki, hata afya yake kwa sasa siyo imara kama zamani. Hivyo, kama ameamua kupumzika sina tatizo naye,” alisema Asha Baraka.
Alifafanua kuwa kuondoka kwa wasanii kwenye bendi ni kitu cha kawaida na kwamba haoni kama kuna jipya zaidi ya kujipanga kwa ajili ya kusonga mbele.
Amigolas alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Twanga Pepeta ambapo alikuwa pamoja na kina Asia Daruwesh, Andy Swebe, Mafumu Bilali, Patrick Kimalee wakati huo ilijulikana kama African Revolution ‘Wana Chumvichumvi’ kabla ya kuja na jina la African Stars Band mwaka 1999.
Kuibuka kwa bendi hiyo kulichangiwa na nyimbo zake zilizofanikiwa kujizolea umaarufu zikiwamo nyimbo za ‘Kisa cha Mpemba’ na ‘Jirani’. Wasanii wanaoweza kujivunia ujio mpya wa Twanga Pepeta katika  mwaka 1999 pamoja na Amigolas ni Luiza Mbutu, Banza Stone, Rogert Hegga (Katapila), Super Nyamwela, Danger Boy, Aisha Madinda, Ally Choki, Yahaya Mkango, Joseph Watuguru, Adolf Mbinga na Ally Akida.
Pamoja na kuwemo katika kila hatua ambayo Twanga imepitia mwanamuziki huyo hana cha kujivunia zaidi ya kuwa maarufu.
Kwa hisani ya Mwananchi

0 maoni: