Saturday 3 August 2013

Meneja wa Wema Sepetu afunguka kuhusu mahusiano yake na Wema

MARA  nyingi amekuwa akionekana karibu sana na msanii wa filamu mwenye jina kubwa Bongo, Wema Isaac Sepetu. Ukaribu wao umewafanya baadhi ya watu kuhisi tofauti.

Wapo waliosema ni wapenzi kutokana na picha zao za kimahaba ambazo wamekuwa wakizipiga na wengine kwenda mbali zaidi ya hapo. Anaitwa Martin Kadinda, mwanamitindo maarufu wa kiume, muanzilishi wa fasheni ya koti aina ya ‘Single Batton’ hapa Bongo.


Huyu ni meneja wa Wema, kwa maana hiyo katika mafanikio ambayo staa huyo ambaye ni Miss Tanzania 2006-07 amekuwa nayo kuna mkono wa Martin. Lakini wengi wamekuwa wakijiuliza, huyu Martin huyu ni nani hasa kwa Wema? Mbona inaonekana kuna lililofichika nyuma ya pazia kati yao? Tumezungumza na Martin na mahojiano hayo maalum yalikuwa hivi;

Ulikutana vipi na Wema?

Ilikuwa mwaka 2006 nilipokuwa nafanya kazi na dada yangu aitwaye Caro kwenye mashindano ya Miss Dar City Centre. Hapo nilikutana na warembo wengi akiwemo Wema. 
Nilipomuona nilibaini ana vipaji vingi, nikahisi anaweza kuja kuwa mtu mkubwa baadaye. Mwaka 2011 akanifuata na kuniambia tufanye kazi pamoja, hapo ndipo ukaribu wetu ulipoanzia.


Wewe ni nani hasa kwa Wema?

Mimi ni meneja wake lakini zaidi ya yote Wema ni best friend (rafiki) yangu na ni mdogo wangu. Nasema hivyo kwa sababu Wema ni pasua kichwa, kufanya naye kazi lazima uweke urafiki kwanza ili muende sawa, hivi hivi ni ngumu.

Mara nyingi mmekuwa mkipiga picha za kimahaba, wewe kama mwanaume hupati hisia za kimapenzi? Watu wanaziita za kimahaba lakini kwetu sisi ni picha za kawaida kwa sababu kiukweli Wema anapenda sana picha za mapozi. Siwezi kusema sijawahi kumtamani Wema, nilishatamani nitoke naye lakini hayo mawazo yalikuwa ni ya zamani. Kwa sasa namchukulia kama ndugu yangu.

Ni kweli huwa unamkuwadia kwa wanaume? 
Siyo ukweli, Wema ni kama dada yangu, nitaanzia wapi kumkuwadia kwa wanaume? 
Unazizungumziaje skendo zake za kila kukicha?
Skendo zake ndizo zilizonifanya nikubali kuwa meneja wake. Nilijua Wema ni biashara, amekuwa akiandikwa sana kwa skendo mbalimbali na akiamka asubuhi bado watu wanamkubali. Kwangu si tatizo sana kwa sababu najua ana mvuto na ndiyo maana kila mtu anataka kujua anafanya nini na ana nini jipya.
Unaweza kulala naye chumba kimoja na msifanye chochote?
Suala hilo ni gumu kulieleza ila haiwezi kutokea tukalala chumba kimoja kwani shetani anaweza kutupitia likatokea la kutokea.

Yapi umemsaidia 
Wema hadi leo?
Nilipoanza kuwa meneja wake nilikuwa na malengo matatu, kumfanya aishi kwenye nyumba ya kistaa, kuwa na kampuni yake pamoja na kumuandalia kipindi cha Reality Show, yote yametimia na mengine makubwa yanakuja.

Ukipewa nafasi ya kumshauri, utamshaurije?
Namshauri kusimama peke yake kama Wema, siyo Wema wa marafiki wala boy friend’s kwani kiukweli wao ndiyo mara nyingi wanamuangusha na kumrudisha nyuma. Naamini kwa akili yake akiwa kama Wema atakuwa mbali sana kwa kuwa ana uwezo wa kufanya mambo makubwa.

Wema amekuwa hadumu na marafiki zake wengi, unadhani ni kwa nini?
Siyo kwamba yeye ana tatizo lakini marafiki anaokuwa nao wengi si wazuri. Naongea hivyo kwa sababu ndiyo ambao wamekuwa wakimgeuka na kumchafua na wakati mwingine kuvujisha siri zake. Kwa sababu Wema ni mtu wa kukasirika mara moja, ndiyo maana hali hiyo hutokea.

Ilishatokea ukagombana na Wema?
Ndiyo! Nilishagombana naye kama mara tatu hivi. Mara ya kwanza nilimwambia ana ‘negative image’, maneno hayo hakuyapenda licha ya kwamba nilikuwa namfikishia ujumbe flani. Mara nyingine ilikuwa kwenye mambo ya kawaida tu ambayo sidhani kama kuna ulazima wa kuyaanika.

Unahisi Wema ana vigezo vya kuwa mkeo?
Ukweli anavyo vigezo vyote, unajua napenda mwanamke mzuri na mwenye akili ingawa hawezi kuwa mke wangu kwa sasa kwa sababu ameshakuwa dada yangu na tayari nina mpenzi ambaye tunapendana sana na tumekuwa tukishirikiana kwenye mambo mengi. Marafiki zangu wa karibu wanamjua.


Kwa hisani ya GPL

0 maoni: