UONGOZI wa Simba umechukua uamuzi wa kumpandisha kizimbani kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa kutokana na uamuzi wake wa kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga. Ngassa aliyekuwa akiichezea Simba kwa mkopo kutoka Azam FC, amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga lakini Simba wamesema walishasaini naye mkataba wa mwaka mmoja.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, Msimbazi wameamua kufanya mambo yao kimya na wameamua kutumia mahakama ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine.
“Hakika sasa tumeona suala hili si la kufanya kama filamu, maana wenzetu (Yanga) pamoja na Ngassa wameamua kutufanyia uhuni. Wachezaji wanataka kufanya Simba ni kama sehemu ya kuchota fedha na kuondoka.
“Kitu kibaya zaidi tumegundua system (mfumo) ya soka imekuwa ikiwalinda sana kutokana na ushabiki mkubwa uliopo katika kamati zilizo chini ya TFF. Sasa sisi tumeona bora kuchukua hatua zaidi,” kilieleza chanzo cha uhakika.
“Tutamfikisha Ngassa mahakamani, tutadai zaidi ya Sh milioni 200 kama sehemu ya kutaka fidia kutokana na mkataba tulioingia naye. Mkataba upo, msione tumekaa kimya mnaona kama hatuna cha kusema.
“Ila sasa tumeamua kufanya mambo kwa mfumo tofauti na leo (jana) usiku tutakuwa na mkutano kwa ajili ya kujadili kuhusiana na suala hili na tutajua lini rasmi apande kizimbani.”
Championi Jumatano ndiyo lilikuwa la kwanza kuandika kuhusiana na Ngassa kusaini Yanga miaka miwili na kueleza kila anachopata katika mkataba wake, achana na wale waliosema katika stori yao eti anatarajia kusaini.
Kwa mujibu wa chanzo hicho kutoka ndani ya Simba, mkataba kati ya Ngassa ulipelekwa na kusajiliwa TFF tangu Desemba, mwaka jana.
Tayari baba yake (soma Uk 2) amezungumzia kuhusiana na mwanaye kuhamahama na Yanga imeshatangaza kumtambulisha kwa mashabiki Juni 3 (soma Uk 2).
Suala la Ngassa kutua Yanga limezua gumzo kubwa na huenda likazua mgogoro mkubwa baina ya timu hizo mbili.
Mwishoni mwa mwaka jana, Ngassa alitua Simba kwa mkopo akitokea Azam, lakini akakabidhiwa gari aina ya Toyota Verossa na Sh milioni 30 na Simba kutangaza imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa mkopo, lakini Ngassa mwenyewe amekuwa akisisitiza hana mkataba na Msimbazi baada ya ule wa Azam kumalizika.
Kwa hisani ya - GLP
0 maoni:
Post a Comment