Friday, 26 April 2013

Mke wa mtu sumu

NI kweli mke wa mtu sumu! Lakini hata mume wa mtu naye sumu! Katika Gazeti la Uwazi ambalo ni ndugu damu mmoja na hili, toleo la 786, Aprili 16-22, 2013 ukurasa wa mbele kulikuwa na habari kubwa; MHESHIMIWA AUMBUKA!


Katika habari hiyo, mtu aliyetajwa kwa jina la Everson Makowa (49) ambaye ni meneja wa kampuni ya kusafirisha mizigo ya Malawi Cargo tawi la mkoani hapa alidaiwa kunaswa gesti na mke wa mfanyakazi wake (jina tunalo).


Sasa, habari mpya ni kwamba bosi huyo ambaye pia ni mbunge mstaafu wa Jimbo la Nkotakota South East nchini mwake anadaiwa kupigwa chini kazini kwake baada ya uongozi wa kampuni hiyo makao makuu yaliyopo nchini Malawi kuzinyaka taarifa za kudaiwa kufumaniwa na mwanamke huyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mara baada ya habari hiyo kutoka kwenye Gazeti la Uwazi na pia kutumbukizwa kwenye mtandao, uongozi wa kampuni hiyo ulimwandikia barua ya kumwachisha kazi mtuhumiwa huyo.

“Amesimamishwa kazi, ile skendo yake ya kunaswa na mke wa mfanyakazi wake ilikuwa mbaya sana, uongozi wa Malawi Cargo nchini mwake ulikasirika sana na kuamua kumpiga chini,” kilidai chanzo.

Paparazi wetu Jumatano iliyopita alikwenda nyumbani kwa mdaiwa huyo ambapo pia ndiko zilipo ofisi za kampuni hiyo kwa lengo la kuzungumza naye lakini watu waliokuwepo walisema alikuwa ametoka.

Kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja (jina lipo) alikiri jamaa huyo kutemeshwa mzigo na kuongeza kuwa, tayari bosi mwingine amefika kuziba nafasi yake. 

Paparazi wetu alipoomba azungumze na bosi mpya, aliambiwa alikuwa na wageni hivyo ikawa vigumu kumpata.

Pamoja na habari ya kutemeshwa kazi, mtuhumiwa huyo ameshindwa kuondoka Mbeya kurudi Malawi kufuatia kesi inayomkabili kutarajiwa kuunguruma mahakamani ambapo mume wa mwanamke huyo ndiye mlalamikaji.

Siku ya tukio, majira ya saa 11:25 jioni, mtuhumiwa huyo alifika kwenye gesti hiyo akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Hilux lenye namba za usajili T 821 ASY.

Mtego wa kumnasa jamaa huyo uliandaliwa na polisi kwa kushirikiana na mume wa mwanamke, jamaa na marafiki huku mke wa mlalamikaji akitoa ushirikiano wa kutosha.

Mwanamke aliyenaswa naye, mumewe alikuwa mfanyakazi wake wa ndani lakini alimsimamisha kazi kwa madai ya kuchelewa kazini.

Habari zinadai, tangu alipomsimamisha alikuwa akiomba penzi kwa mkewe akidai ndiyo ujira wa msamaha kwa mumewe.


Kwa hisani ya - GLP

0 maoni: