Wanaume waamue kupenda na kukubali mitihani ya namna yoyote itakayowakuta wapenzi wao. Wafanye kama alivyoweza Sajuki pale mwenzi wake Wastara alipopata ajali, akakatika mguu. Inawezekana tu kama unakuwa na moyo wa kweli.
Wanawake washike njia ya Wastara. Maradhi au matatizo ya aina yoyote watakayoyapata wapenzi wao, kwao iwe ni changamoto ya kulazimisha kuivuka. Kuna heshima na baraka nyingi katika kufanya kama alivyotenda Wastara kwa Sajuki.
Vilevile, ieleweke kuwa kuna laana katika kumkimbia mwenzi wako pale anapopatwa na matatizo. Hayakuumbwa majanga bila ya kuwepo kwa binadamu. Unaweza kumkimbia mpenzi wako kisa kapata ajali na kutokwa meno, wiki inayofuata nawe yakafika, ukawa chongo.
Mwenzi baadaye anaweka meno ya bandia, anaweza kusimama mbele za watu na kutabasamu, wewe inakuwa ngumu, kwani jicho ndiyo hilo limekwenda zake. Kila mtu akiutakasa moyo wake na akapenda kikwelikweli, mapenzi yatakuwa rahisi mno.
Ni somo tu, watu wajionee maisha jinsi yalivyo. Wakati Wastara anamvumilia Sajuki pamoja na mitihani mikubwa waliyokuwa nayo, wapo wanawake wanaopata kila wanachohitaji, fedha zipo lakini wanasaliti ndoa zao mchana kweupe.
Jiulize wewe ndugu yangu, ni heshima gani ambayo Wastara anapewa leo hii? Kama angemfanyia Sajuki kinyume chake, kwa hakika hivi sasa angekuwa anasemwa vibaya sana. Kinyume cha heshima ni dharau. Nawe unaweza kuamua leo kwamba uheshimiwe au udharauliwe.
Mtu anaweza kudhani kwamba Wastara alimkuta Sajuki akiwa na maisha mazuri pamoja na umaarufu wake. La hasha! Walikutana wakiwa wadogo lakini wakaunganisha ndoto na matarajio ya kufanikiwa pamoja. Malengo yao yalikuwa ya dhati ndiyo maana mwisho wao ukawa huo.
Waliposema “kifo kitutenganishe”, walimaanisha kweli. Mitihani haikuwatenganisha mpaka Sajuki akatangulia mbele ya haki, Wastara akamzika, na sasa anakaa eda. Hicho ni kipimo thabiti kuwa waliamua kupendana kiukweliukweli. Ingekuwa wanafanya utani, wangeachana siku nyingi zilizopita.
Kuuguza ni mtihani mzito hasa pale inapotokea kwamba mgonjwa mwenyewe anakuwa ameugua kwa muda mrefu. Zipo changamoto ambazo hujitokeza ndani, hususan pale mgonjwa mwenyewe anapoathirika kisaikolojia.
0 maoni:
Post a Comment