Thursday 20 December 2012

WEMA asiyesikia la mkuu uvunjika guu ..........

LEO ngoja nimzawadie Wema Isaac Sepetu safu hii kwa kutumia maneno machache lakini naamini ujumbe utamfikia. Sihitaji kumtambulisha Wema kwani jina lake linasimama na kujitosheleza. Ukisikia jina la Wema unawaza nini kwa haraka kichwani mwako? Usinijibu najua simu yangu itajaa ujumbe mfupi au ngoma za masikio yangu zitapasuka kwa kusikiliza simu za wasomaji wangu.
Siku za hivi karibuni kumekuwa na kelele nyingi juu ya marafiki anaokuwa nao kisha hutibuana kwa kashfa na kuacha maneno machafu mtaani. Haileti picha nzuri hasa anapolumbana na marafiki zake wanapotofautiana ambao wao hutumia nafasi hiyo kutangaza majina yao kwa kumdhalilisha kwa maneno machafu.

Wema aliwahi kukurupuka siku za nyuma akatangaza marafiki au mashosti ambao baadaye walimdhalilisha pale tu ushosti wao ulipofikia kikomo.


Aliwahi kukurupuka na kuwa na urafiki mkubwa na waigizaji wenzake, Jacqueline Pentzel ‘Jack wa Chuz’ na Rose Ndauka kwa pamoja bila kujua ‘matabia’ ya Jack wa Chuz ambaye baadaye alitupiana naye maneno makali hadi kufikia kumjumuisha mama Wema, Mariam Sepetu. Haikuleta picha nzuri kwa jamii. Nakumbuka urafiki wao ulidumu hadi ukazaa matunda ya kutengeneza Filamu ya The Diary. Asikwambie mtu, kwenye kolabo hiyo, Rose Ndauka alionesha ukomavu kabla ya kuibuka maneno ya ajabu na mwisho wakasambaratika na kila mtu akawa kivyake.

Baada ya urafiki huo kwenda kaburini, ukafika msimu wa Snura Mushi, Chidy Classic, DJ Choka, Lady Naa, Tiny Dady na wengine wengi ambao nao upepo ulivuma vibaya, damu zikapishana akatibuana nao japo alifanikiwa kutengeneza filamu moja ya The Super Star ambayo haijatoka hadi leo.

Kwa kuwa Snura alitaka jina, basi akaingia kwenye malumbano machafu na Wema akidai kuwa alikuwa na siri zake lukuki alizotaka kuzitoa. Hakuzitoa kwa sababu hakuwa nazo, yalikuwa maneno tu. 

Shetani akapita upepo wa Wema ukavuma kwa mwanamke wa mjini aitwaye Jamilah Msafiri ‘Maira’ wakawa mashosti wa kufa au kupona. Unakumbuka ule msala wa bangi? Huyo ndiye Jamilah ambaye kama ilivyokuwa kwa Snura, hivi karibuni wametibuana kwa kashfa na maneno mbofumbofu.

Kutokana na mifano pamoja na maelezo niliyoyatoa, ningependa kumkumbusha Wema kauli ya mama yake kuwa yeye ndiye rafiki pekee lakini hakuyasikia. Aliziba masikio, hakusikia la mzazi ambaye ndiye mkuu hivyo usemi wa asiyesikia la mkuu huvunjika guu utaendelea kumwandama.

Sipingi mtu kuwa na marafiki bali ni suala la kujiuliza, je, kila mmoja unajua staili za kuishi naye. For the love of game!


Kwa hisani ya - GLP

0 maoni: