Watu wenye silaha wamewateka nyara na kuwauwa waandishi habari wawili wa redio moja ya nchini Ufaransa ambao walikuwa wakielekea kaskazini mwa Mali kwa shughuli za kikazi siku ya Jumamosi(02.11.2013).
Maafisa wa Ufaransa na wa Mali wamesema kuwa watu hao wenye silaha waliwakamata waandishi hao wakati walipokuwa wakitoka katika nyumba ya kiongozi wa waasi.
Vifo hivyo vinakuja siku nne baada ya Ufaransa kusherehekea kuachiliwa huru kwa raia wake wanne ambao wamekuwa wakishikiliwa kwa muda wa miaka mitatu na makundi ya washirika wa al-Qaeda katika eneo la Afrika kaskazini.
Haikufahamika mara moja ni kundi gani limewauwa waandishi habari hao wa radio ya kimataifa ya Ufaransa, Radio France International. Ufaransa ilifanya operesheni ya kijeshi ya kuingilia kati Januari mwaka huu katika koloni lake hilo la zamani kujaribu kuwaondoa wapiganaji wa Kiislamu kutoka madarakani katika mji wa Kidal pamoja na miji mingine katika eneo la kaskazini mwa Mali. Makundi yanayotaka kujitenga sasa yamerejea katika eneo hilo.
Rais asikitishwa
Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameeleza masikitiko yake kutoka na tukio hilo la kuchukiza. Claude Verlon na Ghislaine Dupont walikamatwa na watu kadha wenye silaha baada ya kumaliza mahojiano , amesema afisa mmoja. Miili yao ilitupwa baadaye kilometa kadha nje ya mji katika barabra inayoelekea Tinessako , katika eneo la mashariki ya mji wa Kidal, kwa mujibu wa mtu ambaye aliona miili hiyo na maafisa wanne ambao walielezwa kuhusu suala hilo.
Shirika la utangazaji la RFI limemueleza Dupont mwenye umri wa miaka 51, na Verlon mwenye umri wa miaka 58, kuwa wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu wakiwa na uzoefu wa miaka mingi katika maeneo yenye changamoto. Dupont alikuwa mwandishi habari ambaye "alikuwa anaipenda kazi yake pamoja na bara la Afrika ambapo alikuwa akiandika habari zake tangu alipojiunga na RFI mwaka 1986," shirika hilo limesema katika taarifa . Verlon alikuwa "ameyazowea mazingira magumu duniani kote."
Masikitiko
Wafanyakazi wa shirika hilo, "wameshtushwa mno , wamesikitishwa mno, wamechukizwa na kukasirika," taarifa hiyo imesema. Ufaransa ilianzisha uchunguzi wa kisheria kuhusiana na utekaji nyara na vifo "vinavyohusishwa na makundi ya kigaidi," imesema ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali. Tuhuma katika mauaji hayo ya Jumamosi haraka zimewaangukia wapiganaji wa Kiislamu.
"Kwa taarifa ambazo ninazo , shingo zao zimekatwa. Hatufahamu kwa hakika nani waliowakamata, lakini ripoti tunazozisikia zinaonesha kuwa walikuwa ni makundi ya Waislamu wenye itikadi kali," amesema Lassana Camara , naibu mkuu wa wilaya ya Tinessako.
Maafisa kadha wa Kidal waliohojiwa kwa simu wamesema kuwa waandishi hao wa RFI walikamatwa baada ya mahojiano nyumbani kwa Ambeiry Ag Rhissa, kaimu mkuu wa kundi la harakati za ukombozi wa Azawad, ama NMLA, kundi la Watuareg linalotaka kujitenga ambapo waasi wake walilivamia eneo la kaskazini mwa Mali mwaka jana.
Waasi hao baadaye walifukuzwa kutoka katika eneo hilo la wapiganaji wenye mafungamano na al-Qaeda lakini sasa wamerejea na kulidhibiti eneo la Kidal katika miezi ya hivi karibuni.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri : Bruce Amani
Kwa hisani ya DW
0 maoni:
Post a Comment