Sunday, 10 November 2013

Kocha Fiorentina kutua Azam

  • Stewart Hall asema kilichomuondoa
ALIYEKUA Kocha mshauri wa klabu za Fiorentina na Atlanta za Italia, Fabio Lopez anatarajia kuifundisha timu ya Azam FC ambayo kwa sasa haina kocha baada ya aliyekuwa anaifundisha Muingereza, Stewart Hall kubwaga manyanga. Mtaliano huyo ni mmoja kati ya makocha watatu walioomba kazi ya kuifundisha Azam FC, wengine ni Mromania Dorian Marin na Mcroatia Zdravko Logarusic, aliyewahi kuifundisha Gor Mahia ya Kenya.
Marin aliwahi kuwa kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Eritrea na timu ya taifa ya vijana ya Eritrea ya umri wa chini ya miaka 17.

Azam kwa sasa inafanya mchakato wa kuajiri kocha haraka iwezekanavyo, ili aanze kazi ya kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Hall aliyetangaza kubwaga manyanga juzi, ameeleza sababu za kuondoka katika timu hiyo, akidai amepata ulaji wa nguvu sambamba na mshahara mzuri.

Hall alisema atakuwa mwendawazimu kuacha dili hilo, kwani analipwa mshahara mara tatu zaidi ya aliokuwa analipwa Azam FC.

Alisema amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi katika Timu ya Taifa ya nchi moja kubwa, ambayo hakutaka kuitaja na kulipwa mshahara huo mnono.

“Hii ndio sababu kubwa ya kuamua kuiacha Azam, lakini naondoka nikiwa bado naipenda ila nitakuwa mjinga nikiacha hili dili, kabla ya yote niliongea na uongozi wa Azam kuwaeleza, nashukuru tulikubaliana, hivyo naondoka nikiwa safi.

“Bado nitakuwepo nchini kwa muda wa wiki tatu, halafu nitaenda kuanza changamoto mpya, kwani tayari nimeshasaini mkataba na timu hiyo kama Mkurugenzi wa Ufundi, ila siwezi kusema ni timu gani,” alisema.

Hall alieleza katika kitu ambacho hawezi kukisahau, ni ushirikiano wake na wachezaji wa Azam, anasema hatousahau.

“Nitawamiss, ni wazi nimekuwa nikifurahi kufanya kazi nao, sitawasahau najua tutakutana tena siku nyingine, nawapenda sana,” alisema.

Uongozi wa Azam umebariki kuondoka kwa kocha huyo, huku ukimtakia kila la kheri katika kazi yake mpya.

Kuondoka kwa Hall katika klabu ya Azam si ajabu, kwani Agosti mwaka jana Uongozi wa Azam ulimuondoa mwaka mmoja tangu kuajiriwa kwake, akitoka kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.

Baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.


Kwa hisani ya Mtanzania

0 maoni: