Mahakama nchini Ujerumani imemhukumu jela miaka 14 aliyekuwa meya nchini Rwanda Onesphore Rwabukombe, kwa kuhusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda. Onesphore Rwabukombe mwenye umri wa miaka 56, alipatikana na hatia ya kuamuru mauaji ya mamia ya watu katika kanisa moja ambako walikuwa wametafuta hifadhi katika eneo la Kiziguro.
Alikuwa anaishi kama mkimbizi wa kisiasa nchini Ujerumani tangu mwaka 2002.
Ni kesi ya kwanza kuhusu mauaji ya kimbari nchini Rwanda kusikizwa na kuamuliwa nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kesi hiyo iliyodumu miaka mitatu kabla ya hukumu kutolewa, ilisikiliza ushahidi kutoka kwa watu 100 na majasusi waliokwenda Rwanda kutafuta ushahidi zaidi.
Kesi hiyo ilisikiliza ushahidi kuhusu ambavyo watu 400 na wengine 1,200 waliuawa tarehe 11 mwezi Aprili mwaka 1994, katika kanisa eneo la Kiziguro Mashariki mwa Rwanda ambako Rwabukombe alikuwa meya.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda, yalichochewa na kifo cha hayati Rais Juvenal Habyarimana, aliyeuawa wakati ndege yake ilipodunguliwa karibu na mji wa Kigali mwezi Aprili tarehe sita mwaka 1994.
Muda mfupi baada ya mauaji yake, wanachama kadhaa wa serikali waliokuwa Wahutu wakaanza kupanga mashambulizi dhidi ya watu wa kabila la Tutsi na kusababisha vifo vya watu laki nane.
Kwa hisani ya BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment