Wednesday 18 September 2013

Balozi wa China amefanya makosa makubwa - Waziri Membe

Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, imesema kuwa kitendo kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa Vienna. “Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha Balozi yoyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia,” alisema Membe katika taarifa yake jana jioni.

Taarifa hiyo ilisema kuwa mkataba huo unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na ushabiki wa kisiasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. 

“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa tukio hili Wizara itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,” alisisitiza.

Taarifa hiyo ilisema kuwa Balozi huyo alikwenda wilayani humo kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.

Alisema Wizara imeona picha na habari kwenye vyombo vya habari zikieleza na kumuonyesha Balozi huyo akiwa kwenye mkutano wa CCM.

ALICHOSEMA BALOZI
Balozi huyo amenukuliwa na vyambo vya habari wakati akihutubia mkutano wa hadhara akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kujitahidi kuwasalimia wananchi hao kwa lugha ya kabila la Wasukuma kwa kusema mwadila.

Alisema pamoja na Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, anaamini kuwa CCM bado iko imara na inaweza kuendelea kuongoza kwa muda mrefu.

“Kwa hili inadhihirisha kuwa hakuna chama kama CCM kutokana na uimara wake na hili wanalofanya sasa la kuja kuimarisha chama nasi kule China kupitia chama chetu tawala cha CPC (Chama Cha Kikomunisti cha China), tunafanya kama hivi pia. Mwadila, Shinyanga, CCM Oyeeeeee asanteni sana,” alikaririwa akisema.


Kwa hisani ya Nipashe Jumanne


Vienna Convention on Diplomatic Relations (1961), Article 41: ... 1. Without prejudice to their privileges and immunities, it is the duty of all persons enjoying such privileges and immunities to respect the laws and regulations of the receiving State. They also have a duty not to interfere in the internal affairs of that State ...

0 maoni: