1940: Alizaliwa Kisarawe, Pwani
1960: Alianza muziki
Bendi alizopiga: Kili Chacha, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, DDC Mlimani, Safari Sound na Msondo Ngoma.
Alama na kielelezo cha muziki wa dansi nchini, mkongwe Muhidin Maalim Gurumo (73) wa Bendi ya Msondo Ngoma, ametangaza kustaafu fani hiyo baada ya kutumbuiza jukwaani kwa miaka 53.
Gurumo aliyeimba mfululizo bila kupumzika tangu mwaka 1960, alitangaza azma ya kuachana na muziki jana wakati akiongea na wanahabari kwenye Ukumbi wa Habari, Maelezo, Dar es Salaam.
Mkongwe huyo, alitaja sababu kubwa mbili za kufikia uamuzi huo, kwanza akisema amelazimika kufanya hivyo kutokana na umri, na pili kuwaachia vijana fursa kuendeleza fani pale alipoacha.
Alisema kutokana na umri alionao, imekuwa vigumu kwake kwenda sambamba na kasi, mabadiliko na mahitaji mapya ya muziki huo, hivyo kazi hiyo amewaachia vijana.
“Muziki umekuwa asili yangu kwa muda mrefu, sasa naamua kustaafu ili kutoa fursa kwa vijana kuendelea kupiga muziki huu,” alisema Gurumo na kuongeza: “Nimestaafu muziki, lakini nitaendelea kuwa mshauri.”
“Kwa kipindi chote cha kusimama jukwaani kutumbuiza, mke wangu alikuwa anakosa fursa ya kuwa na mimi kwa sababu ya kurudi usiku wa manane kutoka kazini,” aliongeza Gurumo.
Gurumo aliyezaliwa Kijiji cha Masaki, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, aliwataka vijana wanaokuja nyuma ya muziki wa dansi baada ya kustaafu kwake, kuiga muziki wao ambao umeendelea kudumu na kupendwa mpaka leo.
“Kustaafu kwangu kunakwenda sambamba na kuundwa kamati ya kuangalia jinsi ya kunisaidia kama sehemu ya kuenzi mchango wangu katika fani ya muziki,” alisema Gurumo.
Gurumo alianza muziki na Bendi ya Kilimanjaro Chacha mwaka 1962, kisha Bendi za Rufiji Jazz na Kilwa Jazz kufikia mwaka 1963. Mwaka 1964, alikuwa mmoja kati ya waanzilishi wa Bendi ya Nuta Jazz, ambayo ndiyo ilikuwa kiini cha kuzaliwa Msondo Ngoma.
Pia alikuwa mmoja kati ya wasanii waanzilishi wa Bendi ya DDC Mlimani Park mwaka 1987, kisha Orchestra Safari Sound ‘OSS’, na mwaka 1990 alirudi tena Msondo mpaka alipotangaza kustaafu.
Gurumo ametunga nyimbo nyingi baadhi yake ni pamoja na Ukiwa, Upekepeke si mwema, Rudi Jose, Mwana acha wizi, Mama nipeleke kwa baba na Chatu mkali.
Kwa hisani ya Tumsifu Sanga na Kalunde Jamal, Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment