Saturday, 13 July 2013

Soma habari kamili ya Bibi Harusi aliyeaga dunia dakika 30 kabla ya kufunga ndoa

Bi harusi huyo, Levina Mmassy (23) aliyekuwa mkazi wa Chanika, Handeni mkoani Tanga alifariki dunia Jumamosi ya Julai 6, mwaka huu, majira ya mchana, muda mfupi kabla ya kufunga ndoa na Kasisi Masawe.
PADRI ASUBIRI

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea wakati padri akiwa ameshavaa joho akimsubiri Levina kanisani tayari kwa ajili ya kufunga ndoa hiyo katika Kanisa Katoliki la Handeni.
Nyuma ya tukio hilo, kuna tetesi ambazo hakuna ndugu aliyezizungumzia zinazodai kwamba Juni 26, mwaka huu siku ya sherehe ya send-off iliyofanyika kwenye hoteli moja jijini hapa, bi harusi alipata mshtuko, akaanguka na kupoteza fahamu ukumbini.

RISASI NJE YA UKUMBI!

Kuna madai kuwa baada ya kutokea kutoelewana baina yake na mmoja wa wanafamilia, kulisikika mlio wa risasi iliyopigwa nje ya ukumbi na kusababisha taharuki kwa waalikwa, ndipo Levina akaanguka na kuzimia. 
Ilidaiwa chanzo cha kutoelewana huko ni madai kuwa mwanafamilia huyo alilalamika kupewa pesa kiduchu za ulinzi wa dada yake.

UJAUZITO MIEZI 7

Ilisemekana kuwa mshtuko alioupata bi harusi huyo ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi saba, ndiyo uliosababisha kujifungua kabla ya muda.
Baada ya kujifungua, hali yake haikutengemaa tena hadi mauti yalipomfika ambapo mtoto wake naye alikata roho muda mfupi baada ya kifo cha mama yake.
“Unajua kwetu sisi Wachaga kuna pesa ya ulinzi wa dada pale anapoolewa, huwa inatolewa na bwana harusi…sasa pesa ya ulinzi  iliyotolewa haikuwaridhisha baadhi ya wanafamilia.
“Wakaanza kushinikiza kuongezwa na iliposhindikana mmoja wao aliahidi kuvunja ndoa…vurugu ndiyo zikatokea ukumbini na kusababisha watu kutaharuki na bi harusi kupoteza fahamu,” alidai mmoja wa mashuhuda wetu.

FAMILIA INASEMAJE?
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wanafamilia, Cosmas Mmassy aliliambia gazeti hili kuwa  send-off ya Levina ilifanyika  Juni 26, mwaka huu ambapo harusi yake ilipangwa kufanyika Juni 29, kabla ya kuahirishwa kutokana na sababu za kifamilia na baadaye kupangwa kuwa Julai 6, mwaka huu. 
Mmassy alisema kuwa wakati familia ikiendelea na maandalizi ya harusi, Julai 4, walipata taarifa za bi harusi kwamba alikuwa anajisikia vibaya hivyo jioni ilibidi apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Handeni ambako alilazwa hadi Julai 6 na ulipokaribia muda wa kufunga ndoa, alifariki dunia.

KUMBE NI DAKIKA 20 TU KABLA
“Ndoa ilipangwa ifungwe saa 8:20 mchana lakini alikata roho saa 8:00 ikiwa ni dakika 20 tu kabla ya ndoa na tayari padri alikuwa madhabahuni.
“Unaweza kushangaa lakini ndiyo hali halisi kwa sababu hata muda wa watu kuingia ukumbini wa saa 12:30 jioni  ndiyo miili ilikuwa ikiingizwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga baada ya kusafirishwa kutoka Hospitali ya Handeni… inasikitisha sana,” alisema na kukiri kwamba hilo ni tukio la kwanza kwenye familia yao na hajawahi kuliona. 
“Hii ni miujiza ya aina yake,” alisema Mmassy. 

MKANGANYIKO
Wakati familia ikieleza hayo, watu waliozungumzia tukio hilo mjini hapa  walikuja na mpya baada ya kuleta maswali mengi ambayo hayakuwa na majibu kuhusiana na kifo hicho cha ghafla.

NI MKOSI
Mkanganyiko huo juu ya kifo cha bi harusi huyo na kichanga chake, uliufanya Mji wa Handeni na viunga vyake  kulizungumzia tukio hilo kama sinema huku baadhi ya ndugu wakidai kuwa ni mkosi hivyo kumsaka ‘mchawi’ aliyesababisha nuksi hiyo. 

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wakazi wa Handeni walidai kuwa vifo hivyo vimewaweka kwenye giza totoro na kwamba ili kupatikana undani ni lazima vyombo vya kiuchunguzi viingilie kati.

Wakati  familia ikidai kuwa bi harusi huyo alikutwa na umauti katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni  alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na malaria, baadhi yao walidai  wote wawili walifia nyumbani na si hospitali kama inavyoelezwa.      

DAKTARI ANASEMAJE?
Hata hivyo, kutokana na mkanganyiko huo, gazeti hili liliamua kufuatilia sakata hilo na kuzungumza na daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Dk. Somoka Mwakapalala ambapo alidai kuwa yupo Dar na kwamba hakuwa na taarifa zozote huku akiomba muda afuatilie.
Baadaye Dk. Mwakapalala alikiri kulazwa kwa Levina hospitalini hapo mnamo Julai 4, mwaka huu na kwamba alikuwa akisumbuliwa na malaria kali, iliyosababisha kulazwa kwa ajili ya matibabu na kwamba alifariki dunia Julai  6, akiwa hospitalini hapo.

“Huyu alikuwepo pale hospitali mpaka anafariki dunia, asingeweza kuruhusiwa, ataruhusiwaje na malaria kali?” alihoji na kuongeza:

“Nadhani kuumwa kwake ndiyo chimbuko kubwa la kujifungua mtoto chini ya miezi tisa ambaye naye alifariki dunia pamoja na mama yake.”

HARUSI SH. MILIONI 7.7
Mwenyekiti wa kamati ya harusi hiyo iliyogharimu Sh. milioni 7.7 ambayo ndiyo iligeuka ya mazishi, Abdi Kipacha alisema kuwa ni tukio la kwanza kutokea tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.

ALIKUWA MWALIMU
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu, Levina alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na kwamba alikuwa katika kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti yanamkuta alikuwa hajapokea hata mshahara wake wa awali. 

MAZIKO
Miili ya wawili hao ilisafirishwa Julai 10, kupelekwa kijijini kwao Machame mkoani Kilimanjaro ambako maziko yalifanyika kesho yake.


Angalia picha za mazishi hapa chini
Jeneza la Bi Harisi na Mtoto wake

Ndugu wakiaga mwili

Maiti ikingizwa ndani ya Basi

Kwa hisani ya Dege Masoli/GPL

0 maoni: