Jopo la wanasheria wanaomwakilisha mshambulizi wa Barcelona na Urugua Luiz Suarez limesema linamatumaini makubwa kuwa shirikisho la soka duniani FIFA itapunguza marufuku ya miezi minne aliyopewa mshambulizi huyo baada ya kumngata Giorgio Chiellini.
Luis Suarez mwenye umri wa miaka 27 hajaweza kuingia uwanjani kwa mechi ya aina yeyote tangu mwezi juni shirikisho la soka duniani FIFA ilipompiga marufuku ya miezi minne siku moja baada ya Uruguay kuchuana na Italia katika kombe la dunia huko Brazil.
Kulingana na stakabathi za kesi hiyo ambayo rufaa yake itasikizwa ijumaa katika mahakama ya rufaa ya michezo (The Court of Arbitration for Sport Cas) Suarez anapaswa kupigwa marufuku kushiriki michuano yeyote hadi tarehe 25 mwezi huu .
Mawakili hao wanasema kuwa kwa sababu Suarez alitenda kosa hilo katika mashindano ya kimataifa basi anapaswa kutumikia marufuku ya mechi za kimataifa wala sio mechi zote za kandanda.
Suarez tayari amepigwa marufuku ya kushiriki mechi 9 za kimataifa.
Aidha jopo hilo linatumai litaishawishi jopo la majaji wa mahakama hiyo ya rufaa kumruhusu mteja wao kushiriki mazoezi na klabu yake mpya (Barcelona)huku akiendelea kutumikia marufuku hiyo.
Wakili mkuu wa Suarez, Alejandro Balbi aliiambia runinga moja hugo Uruguay kuwa ni rahisi kupinga marufuku hiyo ndefu ya FIFA kwa sababu inakiuka haki msingi ya mchezaji huyo .
CAS itachukua muda wake kutoa uamuzi wake lakini wandani wanaelezea uwezekano wa Mahakama hiyo ya rufaa ya michezo CAS kutoa uamuzi leo (Ijumaa)
Kwa hisani ya BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment