Sunday, 30 December 2012

Mazito 2012

Hakuna tamu isiyokuwa nachungu! Kwenye ulimwengu wa mastaa Bongo kulikuwa na matukio  ya mengi ya kusikitisha mwaka huu lakini  Yafuatayo ndio mazito zaidi kwa mwaka 2012,Risasi jumamosi lina ripoti kamili. Matukio hayo ya huzuni yamegawanyika makundi tofauti yakiwemo yale ya vifo, kuvunjika kwa ndoa na wengine kutupwa rumande kwa misala mbalimbali.

Said Fundi ‘Mzee Kipara’ na Steven Kanumba enzi za uhai wao
VIFO
Mwaka 2012 umepewa jina la mwaka wa shetani katika sanaa ya Kibongo baada ya kufariki kwa vichwa kibao katika tasnia mbalimbali.
MZEE KIPARA
Mwanzoni mwa mwezi Januari, mwigizaji wa siku nyingi Bongo, Said Fundi ‘Mzee Kipara’ alifariki dunia akiwa kwenye nyumba ya Kundi la Sanaa la Kaole, Kigogo jijini Dar baada ya kusumbuliwa na maradhi mbalimbali yaliyomuandama kwa muda mrefu na utu uzima.


KANUMBA
Aprili 7, 2012, hali haikuwa shwari katika tasnia ya filamu za Kibongo baada ya kufariki kwa ‘legendary’, Steven Kanumba aliyepoteza uhai ghafla baada ya kudondoka nyumbani kwake maeneo ya Hoteli ya Vatican, Sinza jijini Dar.


Mchezaji wa Simba, Patrick Mafisango alivyo pata ajali na gari yake Toyota Crestar Gx 100 hadi umauti wake ulipo mfika kwenye ajali hiyo
MAFISANGO
Mwezi Mei, mwaka huu, sekta ya michezo nayo ilikumbwa na simanzi baada ya mchezaji wa Simba, Patrick Mafisango kufariki dunia kwa ajali iliyotokea maeneo ya Tazara, Dar, wakati akijaribu kumkwepa mwendesha bodaboda ambapo gari lake liliingia mtaroni na hapo ndipo alipopoteza maisha.



MARIAM KHAMIS
Mwezi Novemba kilio kilisikika kwenye muziki wa Taarab baada ya kufariki ghafla kwa staa wa Kundi la Tanzania One Theater (TOT), Mariam Khamis ‘Paka Mapepe’ alipokuwa akijifungua.

MLOPELO
Pia Novemba mwaka huu, mwigizaji aliyepata umaarufu mkubwa enzi za Kaole Sanaa Group kupitia runinga ya ITV, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ alifariki dunia kwenye Hospitali ya Temeke, Dar baada ya kuwa na maumivu ya mwili kwa muda mrefu.


JOHN MAGANGA
Kuonesha kuwa mwezi Novemba bundi alikuwa ameng’ang’ania tasnia ya filamu za Kibongo, pia alifariki mwigizaji John Stephano Maganga baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar.


SHARO MILIONEA
Mwenzi huohuo wa gundu, mwigizaji na mwanamuziki, Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’, alifariki dunia kutokana na ajali ya gari iliyotokea usiku katika eneo la Maguzoni Songa katikati ya Segera na Muheza mkoani Tanga alipokuwa safarini kuelekea nyumbani kwao Muheza kumpelekea mama yake fedha za matumizi.

LULU OSCAR
Pia ndani ya mwezi huohuo, aliyekuwa Mtangazaji wa Kipindi cha Pepeta Afrika kunako SibukaTV, Dar, Lulu Oscar alifariki ghafla akiwa nyumbani kwao Mbezi-Kwayusuf, Dar baada ya kuzidiwa kwa kubanwa na kifua.


AMINA SINGO
Mwezi Desemba, fani ya utangazaji nayo ilipata pigo baada ya kuondokewa na aliyekuwa Mtangazaji wa Kipindi cha Afro-Vibes cha Times FM, Dar, Amina Singo aliyekuwa akiugua kwa muda mrefu.



   NDOA ZILIZOVUNJIKA

UWOYA

Ndoa ya staa wa filamu za Kibongo, Irene Uwoya na mwanasoka wa Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ ilikuwa kwenye msukosuko kwa muda mrefu lakini mwaka 2012 ndipo ule uzi uliokuwa umeishikilia ulidaiwa kukatika.


JACK PATRICK
Modo wa Kibongo, Jacqueline Patrick alifunga ndoa ya kifahari na mfanyabiashara Abdulatif Fundikira lakini ndoa hiyo iliripotiwa kuota mbawa baada ya mumewe kutiwa mbaroni kwa msala wa kusafirisha mihadarati ambaye anaendelea kusota nyuma ya nondo za mahabusu katika Gereza la Keko, Dar.


DIDA
Mwaka 2012, mtangazaji mwenye jina kubwa anayekitumikia kituo cha Radio Times FM, Khadija Shaibu ‘Dida’, alijikuta akirejea kwenye ukapera baada ya ndoa aliyofunga na mwanaume aitwaye Gervas Mbwiga kuvunjika.


HUSNA MAULID
Mshiriki wa Miss Tanzania 2012, Husna Maulid alifunga ndoa na jamaa aliyetajwa kwa jina moja la Aboubakar ‘Abuu’. Hata hivyo, ndoa hiyo haikudumu kwani ilivunjika ndani ya muda mfupi.


TITO
Ndoa ya mwigizaji wa filamu Bongo, Yusuf Zimbwe ‘Tito’, aliyofunga na msichana wa mjini aitwaye Pamela Brown iliota mbawa baada ya kutokea songombingo lenye ujazo mkubwa na kusababisha wawili hao kufikishana mahakamani.


SKAINA
Staa wa filamu, Skyner Ally ‘Skaina’ ndiye ambaye ndoa yake na mwanaume aitwaye Saad Omary ilidumu kwa siku chache kuliko nyingine kwani inakadiriwa kuwa na takriban siku nne huku sababu ikielezwa ni kuolewa kwa staa huyo tayari akiwa na mimba ya mwanaume mwingine.


NORA 
Pia ndoa ya mwigizaji wa kitambo, Nuru Nassor ‘Nora’ na Masoud Ally ‘Luqman’ nayo ilivunjika. Nora alidai kisa cha ndoa kumshinda ni kutokana na mateso ya ajabu aliyokuwa akikutana nayo hasa kutoka kwa ndugu wa upande wa mwanaume. 


WALIOFIKISHWA POLISI
WEMA SEPETU
Katika kuandamwa na makasheshe, mwaka 2012 haukupita hivihivi kwa Wema Sepetu kwani bidada alijikuta akitupwa nyuma ya nondo Mabatini, Kijitonyama, Dar baada ya bangi kukutwa nyumbani kwake. Hata hivyo, soo hilo lilimwangukia shosti wa Wema aitwaye Jamilah Msafiri.


RICHIE
Kaka mkubwa kunako filamu za Kibongo, Single Mtambalike ‘Richie’ alitiwa mbaroni kwa shitaka la kumshambulia mpigapicha wa Kituo cha Runinga cha TBC1 aitwaye Moses.


AUNT EZEKIEL
Mwigizaji Aunt Ezekiel, hivi karibuni alijikuta akisakwa na polisi baada ya kutuhumiwa kumpa kichapo mrembo mmoja kisa kikielezwa kuwa ni mwanaume.


LULU
Mwaka 2012 hautasahaulika kwa Elizabeth Michael ‘Lulu’. Bishosti alitiwa mbaroni na kusota mahakamani kwa msala wa kuhusishwa na mauaji ya mwigizaji Steven Kanumba bila kukusudia.


KAJALA
Staa wa filamu Kajala Masanja alijikuta mikononi mwa polisi hadi leo anasota mahabusu ya Gereza la Segerea, Dar kwa msala wa kuuza nyumba iliyokuwa imewekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), baada ya mumewe kufunguliwa kesi ya kutakatisha fedha haramu.


LORD EYEZ
Rapa Waziri Makuto ‘Lord Eyez’ kutoka Weusi alikamatwa na polisi baada ya kutuhumiwa kujihusisha na wizi wa vifaa vya magari jijini Dar ambapo kesi yake inaendelea mahakamani.


JACK CHUZ
Mwigizaji Jacqueline Pentzel ‘Jack Chuz’ alijikuta akitiwa mikononi mwa polisi katika Kituo cha Pangani, Ilala baada ya kutuhumiwa kuchukua mshiko ili kuongoza filamu lakini mwishoni aliingia mitini kwa madai kuwa aliokuwa akiwaongoza walikuwa wakimdharau.


DIAMOND
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alijikuta matatani polisi baada ya kutuhumiwa kumshambulia mwandishi wa Iringa, Francis Godwin ambapo kesi hiyo ilipofika mahakamani msanii huyo alihukumiwa kifungo au kulipa faini.


SUMA LEE
Mzee wa Hakunaga, Ismail Sadick ‘Suma Lee’, naye mwaka 2012 alijikuta akisakwa na polisi baada ya kutuhumiwa ‘kuchikichia’ mkwanja kwa ajili ya shoo mkoani na kuingia mitini.


0 maoni: