Hilo ni moja ya maagizo yenye utata kuwahi kutolewa chini ya utawala wake, ambapo amekuwa akifanya jitihada za kujijengea mizizi, ikiwamo kuwaondoa na kuwaadhibu wale waliokuwa katika utawala wa baba yake wanaoonekana kutokubaliana na aina yake ya uongozi.
Mapokezi tofauti - Hata hivyo, japokuwa staili yake ya unyoaji wa nywele imekuwa sehemu ya utambulisho wake na inafahamika na kila mmoja, agizo hilo limekuwa na mapokeo tofauti.
“Namna ya unyoaji wake wa nywele inavutia, kwa wanaoipenda. Lakini haiwezi kumpendeza kila mmoja atakayeiiga kwa kuwa maumbo ya vichwa yako tofauti kutokana na maumbile,” alieleza raia mmoja akinukuliwa na Radio Free Asia ya Korea Kusini.
Raia mwingine wa Korea Kaskazini ambaye anaishi nchini China, alieleza kwamba aina hiyo ya unyoaji nywele kwa raia waliopo China inaweza kuonekana kama uhuni.
“Hadi katikati ya miaka ya 2000 tulikuwa tukiitaja aina hiyo ya unyoaji wa nywele kama ‘mtindo wa wahuni wa China,” alisema raia huyu alipohojiwa na gazeti la Korea Times.
Hadi sasa, wanaume wa Korea Kaskazini wana aina 10 za unyoaji zilizowahi kuamriwa na Serikali yao.
Wanaume wamekuwa wakitakiwa kuwa na nywele fupi za wastani zenye urefu wa inchi mbili na wametakiwa pia kuzipunguza kila baada ya siku 15.
Kwa wazee, kwa kiasi fulani wamepewa ahueni kwa kuwa wameruhusiwa kuwa na nywele zenye urefu wa angalau inchi tatu na wanaweza kwenda kwa kinyozi maramojamoja kwa ajili ya kuzipunguza.
Kwa wanawake, wana uhuru zaidi kwa kuwa wana ruhusa ya mitindo 18 ya nywele iliyoamriwa na Serikali ya nchi hiyo.
Kituo cha televisheni ya Serikali ya KoreaKaskazini ambacho kimekuwa kikirusha matangazo yake nchini humo pekee, kimekuwa kikitumika kutoa maelekezo na kueneza kampeni za kutekeleza unyoaji wa nywele katika mtindo huo wanaouita wa Kisoshalisti.
Siyo agizo geni - Mwaka 2005, televisheni ya serikali ilianzisha kampeni maalumu iliyokuwa imelenga kudhibiti aina na namna ya unyoaji kwa wanaume.
Vyombo vya habari vya serikali vilikwenda mbali zaidi kwa kutaka udhibiti zaidi sio tu katika namna ya unyoaji wa nywele, bali pia katika aina na namna ya uvaaji wa nguo.
Aina hiyo ya unyoaji wa Kim Jong –un ilikuwa maarufu katika miaka ya tisini. Baadhi ya watu maarufu hasa wasanii waliitumia kama sehemu ya utambulisho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa, watu wengi nchini Korea Kaskazini hawakuipenda aina hiyo.
Kwa hisani ya Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment