Friday, 6 December 2013

MTOTO wa kwanza wa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amelazwa mahututi katika hospitali iliyoelezwa kuwa katika Mji wa Atlanta nchini Marekani. Taarifa za kulazwa kwa mtoto huyo wa kwanza wa Rage ambaye jina lake halikupatikana mara moja zilianza kuenea juzi na baadaye jana, ambapo watoa habari walieleza kwamba mtoto huyo wa kwanza wa Rage amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kugundulika mwilini mwake kulikuwa na sumu.
“Tumesikia kuwa mtoto wa mwenyekiti amenyweshwa sumu, lakini tumekuwa hatuna uhakika kwa kuwa taarifa tuliyoipata klabuni imeeleza kwamba mtoto wake yuko ICU ingawa hatujui ukweli wa mambo,” alisema mmoja wa wanachama wa Simba.
Taarifa hizo zilienea haraka jana na juhudi za Championi Ijumaa kupata uhakika wa jambo hilo ziliyumba baada ya kila aliyeulizwa wakiwemo viongozi wa Simba kusema pia walikuwa wakilisikia juujuu.
Lakini mmoja wa viongozi wa Simba alisema: “Ukweli ni hivi, mwenyekiti amewatumia email baadhi ya viongozi na kusema mtoto wake huyo yupo ICU, lakini sasa hakuna mwenye uhakika kama ni sumu ingawa wote tumesikia kwamba mwanaye kanyweshwa sumu.”
Alipoulizwa Mjumbe la Baraza la Wadhamini la Simba, Hamis Kilomoni alisema: “Ni kweli nimesikia taarifa hizo lakini sijafanikiwa kuzungumza na Rage mwenyewe.”

Baada ya hapo gazeti hili zikafanyika juhudi kumpata mkewe ambaye yuko jijini Dar es Salaam baada ya simu zote za Rage kutopatikana hewani, simu ilipokelewa na kitinda mimba wa Rage ambaye alisema mama yake ameiacha simu hiyo.


Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, kidogo alionekana kujichanganya ingawa alikiri kuwa kweli kaka yake alikuwa amelazwa nchini Marekani katika chumba hicho cha wagonjwa mahututi.
“Kweli alikuwa amelazwa, lakini leo ametoka na anaendelea vizuri,” alisema na alipoulizwa kuwa kama sumu ilihusika, alijibu:

“Anaumwa pneumonia (rimonia) tu, ingawa sumu imeisha mwilini.” Alipotakiwa kufafanua kuhusiana na sumu iliyoisha mwilini, akaongeza: “Mama akija anaweza kuzungumzia hili.”

Taarifa nyingine zimeeleza kuwa suala hilo limekuwa likifanywa siri kubwa na familia ya Rage ndiyo maana imekuwa vigumu kuliweka wazi. Huku ikidaiwa kuwa kiongozi huyo akitarajiwa kurejea leo Ijumaa.
Rage ana watoto wanne, wa kwanza ni huyo ambaye ni mgonjwa na amekuwa akiishi nchini Marekani wakati wa pili ni wa kike ambaye anaishi nchini Australia. Mtoto wake wa tatu pia anasoma chuo mwaka wa kwanza huko Australia.
Aliyezungumza na Championi Ijumaa ni mwanaye wa mwisho ambaye anasoma sekondari moja maarufu hapa jijini Dar.

POLE:
Kwa niaba ya timu nzima ya Championi, tunamuombea Rage apate ujasiri na nguvu ili apambane katika wakati huu mgumu na kulimaliza tatizo hilo, pia Mungu amsaidie mwanaye kupata nafuu, apone kabisa.
 Kwa hisani ya GPL

0 maoni: