Biashara ya madanguro katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam imeshamiri na kuhatarisha kuporomoka kwa maadili kwa watu wanaoishi jirani na madanguro hayo. Hata hivyo, watu wanaofanya biashara ya kuuza miili yao wanashindwa kuchukuliwa hatua kutokana na kukosekana kwa sheria ya kuwabana. Hatua hiyo imesababisha kampeni za kuwaondoa wamiliki wa madanguro na wanawake wanaofanya biashara hiyo kushindikana kutokana na watu hao kupanga nyumba kama wapangaji wengine.
Jiji la Dar es Salaam limekuwa na ongezeko kubwa la madanguro na baadhi ya hosteli za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kudaiwa kutumika kwa biashara hiyo huku mamlaka zinazohusika kushindwa kudhibiti vitendo hivyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho, Husna Nondo, ambako biashara hiyo imeshamiri, akizungumzia kadhia hiyo katika eneo lake, alisema hakuna sheria inayoruhusu biashara hiyo kuwapo, lakini pia hakuna sheria ya kuwatia hatiani.
“Tumefanya `ambush' mara kwa mara kwa kushirikiana na polisi jamii, lakini mwisho wa siku unajikuta hakuna sheria ya kuwashitaki…” alisema.
Aliishauri serikali kutunga sheria kali dhidi ya vitendo hivyo, vinginevyo maadili yataendelea kumomonyoka kutokana na biashara hiyo kufanywa katikati ya makazi ya watu na wakati mwingine jirani na shule za msingi.
Gazeti hili lilifanikiwa kutembelea eneo la biashara hiyo katika dangulo la Mwananyamala mtaa wa Minazini.
Wanawake wanaofanya biashara hiyo wamekuwa waangalifu wanapopata mwanaume mgeni kwani muda wa maongezi wanachukua tahadhari kubwa kutokana na kuvamiwa mara kwa mara na polisi.
Unapofika nje ya vibanda hivyo, utakutana na wakinadada hao wakiwa wamekaa nje ya vizingiti vya vyumba vyao wakiwa wamevaa kanga moja ama gauni jepesi, unachotakiwa ni kumsabahi na kuingia kwenye chumba alipokaa uliyemkusudia.
Vyumba vyao ni vidogo vyenye kitanda kimoja na baadhi vina televisheni ndogo ambayo hutumika kuweka picha za ngono kwa wateja ambao hisia zao ziko mbali.
Unapoingia ndani ya chumba hicho unakumbana na harufu kali ya manukato ambayo ni zaidi ya udi.
“Gharama zetu ni mazungumzo, lakini kama wewe unataka kulala utalazimika kuniachia Sh. 10,000 na uje kuanzia saa nne usiku kwa vile huu muda wa katikati bado tunahudumia wateja wengine,” alisema dada huyo.
Dada huyo mwenye umri wa kati ya miaka 20 na 30, aliyekataa kutaja jina lake, muda wote wa maongezi alionekana mwenye uzoefu na anachozungumza.
Alisema chumba kimoja kinaweza kutumiwa na zaidi ya wasichana watatu na huwa wanaingia kwa zamu kwa kuwa wana makazi yao nje ya maeneo hayo ya biashara na wanafamilia zao.
Msichana huyo baada ya kukubaliana na mwandishi wakutane usiku, hakutaka tena mazungumzo kwani muda wote alikuwa akifunua pazia la chumba chake ili asipitwe na mteja na kumtaka mwandishi aondoke.
Akizungumzia mazingira ya biashara hiyo, Ofisa Mtendaji huyo alisema harufu kali iliyomo ndani ya vyumba hivyo ni kwa ajili ya kusafisha uvundo unaotokana na wasichana hao kuhudumia wanaume zaidi ya mmoja kwa muda mfupi.
Alisema katika kata yake vipo vyumba zaidi ya 80 vinavyotumiwa na wafanyabiashara hiyo haramu.
“Unajua ukizungumza nao, hii biashara inawalipa sana, wengine wanasomesha watoto wao na wanaweza kulipa kodi ya Sh. 150,000 kwa mwezi na wakati mwingine kwa siku wanaweza kukusanya mpaka Sh. 70,000,” alisema.
Nondo alisema biashara hiyo haramu ambayo ilikuwapo tangu miaka ya 1980, inahitajika jitihada za busara na si nguvu katika kuitokomeza.
“Kuna haya mashirika ya kijamii hasa yanayoshughulika na masuala ya uzazi na ukimwi, wanatakiwa kujikita kwa kundi hilo kutoa elimu ya athari za biashara hiyo, vinginevyo jitihada za serikali za kutokomeza magonjwa ya zinaa na ukimwi hazina maana,” alisema.
Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walionyesha kushangilia kuwapo kwa biashara hiyo kwa kile walichodai kuwa matukio ya ubakaji yamepungua.
Hata hivyo baadhi walilaani kwa maelezo kuwa maadili yanatoweka kwa kuwa biashara hiyo inafanywa waziwazi katikati ya makazi.
kwa hisani ya NIPASHE JUMAPILI
0 maoni:
Post a Comment