HUWEZI kuacha kutafsiri kwamba, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda anawahenyesha askari wa Dar es Salaam tena kwa saa 24, Ijumaa Wikienda limegundua. Hali hiyo imesababishwa na ulinzi mkali anaotakiwa kupewa Shehe Ponda na askari wa jela kwenye Magereza ya Segerea, Dar baada ya kupokea mzigo huo wa kumlinda kutoka kwa askari polisi na usalama wa taifa alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili.
Wiki mbili zilizopita akiwa kwenye mhadhara mjini Morogoro, Shehe Ponda alidai kupigwa risasi kwenye bega la kulia. Wakati wa tukio hilo, Ponda alikuwa akisakwa na polisi kwa kosa la kutoa hotuba yenye uchochezi akiwa Zanzibar huku akijua yupo ndani ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambacho kinataka asipatikane na shitaka.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar, afande mmoja kutoka jeshi la polisi (aliomba hifadhi ya jina) alisema polisi wanamshukuru Mungu Ponda kupelekwa Seregea, wenzao wa magereza nao wakahenyeshwe na ulinzi.
“Unajua nini ndugu mwandishi? Kumlinda Ponda ni kufa na kupona, popote unapokuwa naye, wenzake wanaweza kuvamia na kuvunja amani, wewe una bunduki wao hawana silaha, unafanyaje hapo?” alisema afande huyo.
Uchunguzi zaidi wa Ijumaa Wikienda umebaini kuwa, baadhi ya askari polisi walikuwa wakikwepa kushika zamu ya kumlinda Ponda Muhimbili kwa kuona ugumu wa kudhibiti vurugu endapo wafuasi wake wangeamua kukinukisha.
Mei 9, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilimhukumu Ponda kifungo cha nje cha mwaka mmoja jela. Ponda na wafuasi wake 49 (waliachiwa huru) walidaiwa kakaidi agizo la jeshi polisi kwa kufanya maandamano haramu Februari 15, mwaka huu kwenda katika ofisi za DPP.
Kwa hisani ya GPL
0 maoni:
Post a Comment