Mahakama moja nchini Italia inatarajiwa kuamua ikiwa aliyekuwa waziri mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi alilipia ngono na kahaba aliyekuwa na umri mdogo pamoja na kutumia mamlaka yake vibaya kama waziri mkuu. Inadaiwa Belusconi alilipa pesa ili kununua huduma za kahaba huyo Karima El Mahrou raia wa Morocco mwaka 2010 wakati huo akiwa na umri wa miaka 17.
Viongozi wa mashtaka katika kesi hiyo mjini Milan wanataka Berlusconi afungwe jela miaka sita pamoja na kuzuiwa kabisa kushikilia wadhifa wowote wa kitaifa.
Belusconi ambaye ni tajiri mkubwa na mmiliki wa vyombo vya habari Italia, anakanusha madai hayo.
Aidha Berlusconi, ambaye anakumbwa na kesi nyingi mahakamani alifungwa jela kwa miaka minne kwa kukwepa kulipa kodi mwezi Oktoba mwaka 2012.
Ombi lake kwa mahakama kutupilia mbali uamuzi wake liligonga mwamba wiki jana.
Uamuzi wa kesi hiyo huenda ukaathiri pakubwa mustakabali wa kisiasa wa Berlusconi.
Viongozi wa mashtaka mjini Milan wanasema kuwa wanawake walikuwa wakialikwa nyumbani kwa Berlusconi kwa ajili ya kusherehekea kwa kile kilichojulikana kama "bunga-bunga" yaani sherehe za makahaba na Berlusconi kwa muda mrefu, walikuwa sehemu ya mtandao wa makahaba nawalikuwa wanatumiwa na Berlusconi kujinufaisha kingono.
Hata hivyo Berlusconi na msichana huyo wamekanusha madai hayo. El Mahroug alisema kuwa alipokea pauni 5,900 lakini ilikuwa kama zawadi.
Kwa hisani ya BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment