Wednesday, 22 May 2013

MWAKIFWAMBA: Wanaovaa VIMINI kwenye filamu wanajiuza

RAIS wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifwamba amesema wasanii wanaovaa mavazi yasiyo na staha ikiwemo vimini kwenye sinema wanajiuza. Mwakifwamba aliyasema hayo katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa ameongozana na msanii Riyama Ally. Kauli hiyo ya Mwakifwamba imekuja siku chache baada ya sakata la uvaaji vimini na udhalilishaji wanawake na wototo kwenye filamu kuzungumziwa bungeni, Dodoma. 
APIGIA MSUMARI
“Hili suala nimeshalikemea kwa muda mrefu sana... naamini kama ni watu wa kuelewa watakuwa wameelewa na wale ambao wanaendelea na hayo mambo maana yake ujue wana mambo yao.

“Siyo wote wanaoingia kwenye filamu ni wasanii wa kweli, wengine wanatumia tasnia hii kutafuta mabwana ndiyo maana wanavaa mavazi ya ajabu ili waonekane, jambo ambalo tunalikemea kila wakati.

“Sikatai wakati mwingine kuna ‘scene’ zitahitaji uhusika fulani kama uchangudoa lakini utakuta msanii anatakiwa kuvaa uhusika wa ofisini, yeye anavaa vinguo vya hovyo, maana yake ni nini kama si kutafuta soko?” alisema Mwakifwamba na kuongeza: “Imefika wakati wasanii wanatakiwa wabadilike kwani hali ilipofikia siyo pazuri. Bado msanii anaweza kuonekana ana kiwango kizuri bila kuvaa nguo zinazomdhalilisha na kumtafsiri vibaya mbele ya jamii.”
Akasema: “Sasa nasema hivi, yeyote atakayekiuka utaratibu tuliokubaliana tutamchukulia hatua. Hatutamfumbia macho. Tunahitaji kuwa na tasnia yenye heshima.”

RIYAMA SASA
Mkali wa kucheza na hisia, Riyama naye alitoa maoni yake kuhusu mavazi na mwenendo mzima wa filamu za Kibongo ambapo kwa upande wake alisema anaamini wanaofanya hivyo wanatafuta kuwa mastaa kwa njia ya mkato.

“Tatizo ni ulimbukeni wa kuiga wasanii wa nje. Wasanii tunakiwa kujitambua na kufahamu na kulinda utamaduni wetu. Wasanii wengi hawajui thamani zao, jamani ustaa siyo kukaa uchi.

“Tujue kuwa kwenye filamu siyo sehemu ya kutafutia mabwana. Kuonesha urembo wetu wa nje na wa ndani kwenye hadhara siyo kitu kizuri kwa utamaduni wetu... hao wanaofanya hivyo wanasababisha wasanii wote tuonekane machangudoa,” alisema Riyama.

Kwa hisani ya - GLP


0 maoni: