Thursday, 30 May 2013

Ama kweli mjini shule! Ombaomba feki anaswa live....

WAKAZI wa mjini Iringa hivi karibuni wameshuhudia kituko cha mwaka baada ya kumnasa mzee mmoja akijifanya ombaomba kwa kuigiza ulemavu asiokuwa nao. Ombaomba huyo feki alijifanya hana mkono wa kushoto na mguu wa kulia na kuweka pozi la kuomba kama vile ni mlemavu katika eneo la Hazina Ndogo, mjini hapa. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mlemavu huyo feki ameumbuliwa na mtu mmoja ambaye alimuona asubuhi ya siku ya tukio akiwa hana ulemavu wowote kabla ya kumkuta mchana akiomba kwa kujifanya ni mlemavu wa mkono na mguu.
Mtu huyo aliwaambia baadhi ya wananchi siri ya ombaomba huyo na kuwafanya kupandwa na hasira na kuanza kumshushia kipigo wakitaka kuhakikisha kama kweli ni mzima kiasi cha kumuumiza usoni.

Kwa hofu ya kuuawa, mlemavu huyo feki alijinusuru kwa kuonesha mkono wake wa kushoto aliokuwa ameuficha ndani ya koti alilolivaa na mguu aliokuwa ameukunja na kuukalia.


Wakati wananchi wenye hasira wakiendelea kumpiga, mzee huyo alijitahidi kupata upenyo na kutimua mbio ndefu kukimbilia eneo la Miyomboni na kuwaacha watu wengine wakiwa hawana mbavu kwa vicheko.


Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walipoongea na mwandishi wetu walisema wakati mwingine ombaomba huyo hujifanya bubu na kuwaomba watu fedha za matibabu.


Inadaiwa kuwa hii si mara ya kwanza kwa ombaomba huyo kushtukiwa akifanya mchezo huo, awali alishawahi kufukuzwa katika Kitongoji cha Santoni mjini hapa.

“Bahati yake amekimbia kama tukimkuta tena akijidai ni mlemavu tutamvunja mkono na mguu ili awe mlemavu kweli,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo. 


Tuhuma nyingine zinasema kuwa ombaomba huyo hutumia mbinu hizo za kitapeli kwa kuwa amekimbiwa na mpenzi kutokana na kutokuwa na kipato.

Wananchi hao wenye hasira wameutaka uongozi wa Manispaa ya Iringa kuwabana ombaomba wote wanatumia udanganyifu kujipatia fedha na kutaka kuwepo kwa utaratibu maalum wa kuwasaidia wanaohitaji misaada ya kweli.

Angalia picha zaidi za tukio hapa chini





Kwa hisani ya GLP

0 maoni: