Tuesday, 16 April 2013

Haponi mtu

IMEBAINIKA kwamba kuna mtandao wa askari ndani ya majeshi mbalimbali ya ulinzi nchini na hasa Jeshi la Magereza ambao unajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Uchunguzi wa Uwazi umebaini kwamba tayari orodha ya majina ya askari hao yamekabidhiwa kwa Kamishna Jenerali Mkuu wa Magereza, John Minja ili kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa chanzo makini kilichopo ndani ya jeshi hilo, kilisema kwamba tayari mkakati maalum umeandaliwa ili kuwachukulia hatua askari wanaojihusisha na mtandao huo na kuahidi kwamba hakuna mtu hata mmoja atakayepona.

“Taa nyekundu imewaka kwani baada ya kamishna kupata orodha hiyo aliweza kuwapangua askari wakubwa katika Gereza la Keko jijini Dar na kuwatawanya sehemu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba mtandao huo unakoma na biashara hiyo inafikia tamati.

“Pia, makachero makini wamewekwa  katika kila gereza hapa nchini ili kupambana na hali hiyo na majeshi yote yatachunguzwa,” kimesema chanzo  hicho.

Mkakati huo uliandaliwa kabla ya  Aprili 7, mwaka huu ambapo  saa 4 usiku makachero  walimnasa askari magereza, Brighton Octavian, akiingia kazini katika Gereza la Keko  akiwa na kete  732 za Heroin kwa  madai ya kuzipeleka kwa wafungwa.

Imedaiwa kuwa askari huyo ni mmoja tu  kati ya watu wanaodaiwa kuunda mtandao huo ambao pia unawashirikisha baadhi ya raia na vigogo wa madawa ya kulevya hapa nchini.

“Kamishna Minja amethubutu kuchukua hatua ili kurekebisha tabia na mwenendo wa magereza yetu kwa kuwa  huko nyuma hali ilikuwa mbaya na kuonekana kama sehemu ya genge la kupitisha madawa ya kulevya kwa ajili ya wafungwa,” kilisema chanzo hicho.

Uwazi limebaini kwamba baadhi ya askari katika magereza mbalimbali nchini wamekuwa na maisha mazuri kuliko makamishna wa magereza, hali ambayo inawashangaza wengi.



Inadawa kwamba askari hao wamekuwa si waaminifu kutokana na kushiriki kwao katika mtandao huo wa biashara haramu.

Baada ya Kamishna Minja kuteuliwa kuongoza jeshi hilo, aliunda tume ya kuchunguza changamoto mbalimbali na kugundua udhaifu mkubwa katika Gereza la Keko.

Gazeti hili lilimsaka Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa na kumuuliza hatua wanazozichukua kutokana na hali hiyo.

Mbali na kumtaja askari magereza Brighton, pia Nzowa aliongeza kuwa wapo katika mpango maalum wa kumaliza tatizo hilo ndani ya magereza nchini.

“Askari aliyekamatwa alikutwa na kete 732, tunajipanga kuumaliza mtandao wao kwa nguvu zote,” alisema Nzowa na kuongeza kuwa inashangaza kuona askari nao wameingia kwenye biashara hiyo haramu.

Alipoulizwa kuhusu majeshi mengine, Nzowa alisema wakuu wake ambao ni wa majeshi yote hawataki kabisa kuona biashara hiyo haramu inafanyika popote pale, hivyo yupo nao bega kwa bega kupambana na askari atakayethubutu kuifanya.

Naye Msemaji wa Jeshi la Magereza, Mtiga Omari alisema askari Brighton ameshafukuzwa kazi.

“Tumemkabidhi kwa polisi ili ashughulikiwe kisheria na kuhusu majina ya baadhi ya askari wengine wa magereza wanaojihusisha na biashara hiyo naomba unipe muda nifuatilie,” alisema Kamanda Mtiga.

Jeshi la polisi linaongozwa na IGP Said Mwema na kanda maalum inaongozwa na DCP Suleiman Kova ambao wote wapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Dk Emmanuel Nchimbi ambaye kasi yake ya utendaji kazi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete, inasifiwa na wengi.

Kwa hisani ya GLP

0 maoni: