Saturday, 9 August 2014

Adaiwa kumdhalilisha mfanyakazi


Hai. Mkazi wa Singida Mjini, Jacqueline Kweka (30) jana alipandishwa mahakamani mjini hapa akikabiliwa na tuhuma za kumfanyia ukatili mfanyakazi wake wa ndani (15).

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akimpiga mfanyakazi wake huyo sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo kumvuta nyama za sehemu za siri kwa kutumia bisibisi.

Baada ya tuhuma hizo kuibuliwa na raia wema, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka Singida na kukimbilia kijiji cha Narumu wilayani Hai, Kilimanjaro alikokamatwa baada ya taarifa kuvuja.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi, Mfawidhi wa Wilaya, Denis Mpelembwa na kukanusha mashitaka dhidi yake. Hati ya mashtaka hayo ya kujeruhi mfanyakazi wake huyo ni ya awali ili kuruhusu polisi kutoka Singida kwenda kumchukua mtuhumiwa huyo.

Akimsomea mashitaka, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Marwa Mwita alidai mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo Julai mwaka huu siku tofauti.

Mtuhumiwa huyo alikanusha mashitaka hayo na amerudishwa rumande hadi Agosti 21 wakati ukisubiriwa utaratibu wa kumsafirisha kwenda Singida.

Msichana anayedaiwa kufanyiwa ukatili huo, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa matibabu na taarifa zinadai amepoteza uwezo wa kusikia na hapati tena siku zake za hedhi na amelazwa hapo kwa wiki ya pili sasa.

Hivi karibuni matukio ya kunyanyasa wafanyakazi wa ndani yamezidi kushika kasi likiwamo lile la msichana, Yusta Lucas (20) anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi mwili mzima na mwajiri wake Amina Maige, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Mwanamke huyo ameshtakiwa  kwa kosa la kumjeruhi mfanyakazi wake huyo kwa kumng’ata sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha makubwa.

Kesi hiyo ambayo imeendelea kuvuta hisia za watu wengi kila iitwapo, inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Baadhi ya watu wanaozungumzia unyanyasaji wa aina hiyo, wanataka upigwe vita na jamii.

Kwa hisani ya Mwananchi

0 maoni: