Saturday 11 January 2014

Askari JWTZ kizimbani kwa mauaji

ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Rashid Mzee Abdalla (43), mkazi wa Mtoni Kijichi, amepandishwa kizimbani kwa makosa ya kuua watu wawili. Rashid alifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Ester Mwakalinga. Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, alidai mahakamni hapo kuwa matukio hayo yalitokea Januari Mosi, mwaka huu, katika mkesha wa wa Mwaka Mpya, maeneo ya Pugu Kwa Mustafa, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.


Wakili Nassoro alidai kuwa mshitakiwa aliwaua watu wawili ambao ni Abubakar Hassan na Ibrahim Mohamedi. Ilidaiwa kuwa matukio hayo mawili yalifanyika kwa wakati mmoja na eneo hili lililotajwa.

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 29, mwaka huu kwa kutajwa.

Wakati huo huo, mkazi wa Masaki Jeshini, Sakila Peter (19), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na shitaka la kumjeruhi Labii Segumba kwa kutumia kipande cha chupa.

Akisomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Jackline Rugemalila, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Mwanamina Komakono, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 29, mwaka jana, eneo la Oysterbay.

Hata hivyo, mshitakiwa alikana kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana hadi Januari 21, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.


Kwa hisani ya Mtanzania

0 maoni: