Maharusi katikati wakiwa katika picha ya pamoja na wazazi wa bibi harusi (kushoto) na wazazi wa bwana harusi (kulia).
UNAWEZA kusema ni jeuri ya fedha baada ya mwanamke, Rukia Apach kukubali kulipa shilingi milioni 4 ili apewe talaka na mumewe, Mohamed Kismati baada ya kuzuiwa kufanya kazi na mkwewe, Ijumaa linakunyetishia. Ndoa hiyo ilifungwa miaka miwili iliyopita na kufuatiwa na sherehe ya kifahari katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar mwaka juzi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wawili hao wameachana kwa madai kwamba baba mkwe wa Rukia kukataa mkwewe huyo afanye kazi zaidi ya kuwa mama wa nyumbani.
Akizungumza na Ijumaa, Rukia alisema kwamba mumewe alimuahidi kumwendeleza kielimu wakati alipokuwa akisoma kidato cha sita pindi akimuoa.
“Awali mume wangu aliniahidi kuniendelea kimasomo, lakini baada ya kuolewa nikakataliwa hata kufanya kazi, amri ambayo ilitolewa na baba mkwe wangu ambaye ni mfanyabiashara,” alisema Rukia.
Mwanamke huyo alidai kwamba familia ya mumewe ilishikilia msimamo huo hadi ndoa yao ilipovunjika hivi karibuni.
Kama vile haitoshi, Rukia amedai kuwa alilazimika kulipa baadhi ya vitu na kutoa kiasi cha shilingi milioni 4 ili aweze kupewa talaka yake.
Rukia alidai kwamba chanzo cha yote kilianza baada ya baba mkwe wake kwenda Dubai kuangalia biashara zake, naye kuutumia mwanya huo kumuomba ruhusa mumewe ili akafanye kazi na kukubaliana ndipo alipoanza kazi Mlimani City, jijini Dar.
Hata hivyo, baba mkwe aliporeja akakipinga kitendo hicho na kumwambia mwanaye kwamba kumruhusu mkewe kufanya kazi ni sawa na kumtoa sadaka kwa wanaume wengine.
“Niliomba ruhusa ya siku tatu kazini ili nipate muda wa kuzungumza hilo na mume wangu lakini ilishindikana, nikaamua kurudi kazini,” aliendelea kusema Rukia.
Mwanamke huyo alisema kwamba baada ya kurudi kazini, familia ya mumewe ilimnunia na kumtaka kuondoka huku wakimzuia kuingia chumbani kwake.
“Waliniambia mizigo yangu wataniletea, nikaondoka na kurudi kwetu,”alisema Rukia kwa majonzi.
Pamoja na familia hizo kukutana na kulizungumzia jambo hilo, lakini mwafaka ulishindika ndipo upande wa mumewe ulipodai kulipwa shilingi milioni 7 kama gharama za mahari yao ili watoe talaka.
“Sikuolewa kwa pesa hizo, tukalifikisha suala hilo Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) na kukubaliana kuwalipa shilingi milioni 4 hivyo ikawa kama nimeinunua talaka yangu,” alisema Rukia.
Mume wa Rukia, Mohamed alikiri kutokea kwa jambo hilo na kusisitiza kuwa alimuoa mwanamke huyo na hivyo alipaswa kufuata matakwa yake, vinginevyo ndiyo sababu kubwa ya kumuacha.
Familia hizo zilikutana Bakwata Jumatatu iliyopita na Rukia akakabidhiwa vitu vyake alivyoviacha kwa mumewe pamoja na pete ya ndoa.
Tafrani ilizuka baada ya mama mkwe kudai arejeshewe pete aliyovikwa mke huyo siku ya harusi, akimwakilisha mwanaye ambaye hakuhudhuria kikao hicho.
Shehe wa Bakatwa (jina halikupatikana) aliwataka kukubaliana na aya ya 20 katika Surat Nisai ambayo inakataza kumdai mali yoyote ile uliyomzawadia mkeo.
“Mlioana kwa hisani na muachane kwa hisani isitoshe unapomuacha umeshamtumia si vyema kumdai mali uliyotoa,” alisema shehe huyo.
Picha zaidi fungua hapa - GPL
0 maoni:
Post a Comment