Thursday, 21 November 2013

DC wa zamani kortini kwa ubadhirifu wa pembejeo

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani hapa, imemsomea mashtaka aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Hadija Nyembo, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hamida Kwikwega, kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za pembejeo. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Chato vocha za pembejeo za ruzuku zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5 kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya wakulima na kuongeza tija.

Mbali na vigogo hao, wengine waliosomewa mashtaka mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Chato ni Ofisa Kilimo na Mifugo wa wilaya hiyo, Dk. Phares Tongola, Mary David (wakala wa usambazaji wa pembejeo za kilimo kata ya Buseresere) na Mageni Mbassa (Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Mapinduzi) wilayani hapa.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Kelvin Murusuri, alidai kuwa watuhumiwa namba nne na tano ambao ni wakala wa usambazaji wa vocha za pembejeo kata ya Buseresere na Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho, wanakabiliwa na makosa 60 yakiwamo ya kughushi na kutenda makosa kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

Aidha, alidai kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Nyembo, aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kwikwega na Ofisa Kilimo na Mifugo, Dk. Tongola, wanakabiliwa na makosa matatu kila mmoja likiwamo la kutumia madaraka yao vibaya kisha kumteua wakala wa usambazaji wa pembejeo asiye na sifa.

Mengine ni kufanya ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kutumia nafasi zao kumsaidia kutenda kosa wakala wa usambazaji wa pembejeo hizo huku wakijua wazi kuwa ni kosa.

Mwanasheria huyo alisema washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 10, mwaka 2010 na  Januari mosi, mwaka 2011 na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yao.

Mwendesha Mashtaka, aliiomba mahakama hiyo kukubali kesi hizo kuanza kusikilizwa kwa hatua ya awali leo, ombi ambalo lilikubaliwa.

Hakimu wa mahakama hiyo, Jovith Katto, alisema kutokana na upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wao, kesi hiyo itaanza kusikilizwa leo kwa hatua ya awali na kwamba dhamana za watuhumiwa zinaendelea.
SOURCE: NIPASHE

0 maoni: