Wednesday, 3 July 2013

Washitakiwa wa Kesi ya mauaji ya Mwanahabari Daudi Mwangosi waachiwa huru

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mufindi imetupilia mbali mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Hamad Yusuph na wenzake 42.  Kiongozi huyo pamoja na wenzake walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo la kufanya mkutano bila kibali pamoja na kuharibu mali ambazo ni kofia za pikipiki (helmenti) 2 za polisi katika tukio lililosababisha kuuawa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten Daudi Mangosi katika kijiji cha Nyololo wailayani Mufindi. 
Kutokana na tuhuma hizo Chadema iliweka pingamizi za kutaka kesi hiyo ifute kwa kuwa ilifunguliwa kinyume cha sheria.
 
Wakili wa Chadema Lugaziya akisaidiana na mwanasheria wa Chadema Luka Sinkala Mwenda waliweka pingamizi dhidi ya  kesi hiyo .
 
Pingamizi lingine ni kwamba aliyetoa amri ya kutawanya mkutano hakuwa na cheo chochote, wakati Chadema ikizuiliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Bububu Zanzibar walikuwa na mkutano wa kampeni za uchaguzi, polisi walisema wanazuia mkutano kwa kuwa sensa inaendelea wakati huo sheria ya uchaguzi haizuii shughuli zingine kufanyika na kwamba walitaka polisi waeleze sheria ya sensa inayozuia shughuli zingine kufanyika inatoka wapi.
Watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Igawa mpakani mwa Mkoa wa Iringa na Mbeya baada ya kutoka katika eneo waliloamriwa kutawanyika.
Hakimu wa Wilaya ya Mufindi D. Nyakunga alisema pingamizi zilizowasilishwa na Chadema hazikujibiwa hata moja na upande wa utetezi.
 
"Hakuna pingamizi yoyote iliyojibiwa na upande wa utetezi. hivyo na kuwa hayo  ni matumizi mabaya ya kifungu namba 91 kinataka upande wa utetezi kujibu pingamizi.
"Pia ni matumizi mabaya ya muda na fedha za serikali za walipa kodi. Kwa sababu zote hizo, kesi hii inafutwa" alisema Nyakunga.
 
Naibu Katibu Mkuuwa wa Chadema Zanzibar Hamad Yusuph na wenzake walifunguliwa kesi hiyo baada ya kukamatwa wakati wa ufunguzi wa matawi Septemba 2, 2012 ambapo mwanahabri  wa Chanel Tena na mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa  wa Iringa (IPC) Daud Mwangosi aliuawa na polisi kwa kupigwa bomu.

Kwa hisani ya Gustav Chahe, Mufindi

0 maoni: