Wednesday, 3 July 2013

NGASSA akata Mzizi wa Fitina...... atua Mazoezini Yanga

HATIMAYE kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa (pichani), amekata mzizi wa fitna baada ya kuanza kujifua rasmi na timu hiyo, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu asajiliwe. Awali kulikuwa na utata wa mchezaji huyo ataichezea timu gani kati ya Simba na Yanga ambazo zote zilikuwa zinadai kuwa zina mkataba na kiungo huyo, ilifika mbali mpaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilisema kuwa bado linautambua mkataba wa Simba na mchezaji huyo mzaliwa wa Mwanza.

Lakini jana alionekana ni mchezaji wa Yanga baada ya kumaliza mkataba wa mkopo akitokea kwenye kikosi cha Azam aliokuwa akiutumikia kwenye kikosi cha Simba kutokana na kuwasili kwenye mazoezi ya Yanga ikiwa ni siku ya kwanza tu ya mazoezi ya Wanajangwani hao kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na Klabu Bingwa Afrika.

Ngassa alitua jana asubuhi katika mazoezi ya timu hiyo yaliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, ambapo mara baada ya kuwasili, alikutana na kocha wa kikosi hicho, Ernie Brandts.

Mara baada ya kukutana na Brandts, Ngassa ambaye ametokea kwenye kikosi cha Simba, alisalimiana naye kwa dakika moja kabla ya kujumuika na timu nzima katika kuomba dua na kuanza mazoezi.

Mara baada ya dua hiyo iliyochukua dakika tano, Championi Jumatano lilimshuhudia Brandts akimtambulisha nyota huyo kwa wachezaji wote, huku akiwataka nyota wengine kumpa ushirikiano na baadaye kiungo huyo akaanza kusalimiana na wenzake walioonyesha furaha kumuona.

Championi lilikuwa gazeti la kwanza kutoa taarifa ya nyota huyo kusaini Yanga, kabla ya uongozi wa timu hiyo kumtambulisha rasmi mwezi mmoja uliopita.

Mara baada ya Ngassa kusalimiana na wenzake, alianza kujifua rasmi katika zoezi la kupasha misuli moto, ambapo nyota wote walikimbia kuzunguka uwanja mzima, kabla ya kuhamia katika zoezi la mbio fupi za kasi.

Kivutio kikubwa kikiwa ni jinsi kiungo huyo alivyokuwa akionyesha bidii katika mazoezi yote aliyokuwa akiyafanya.

Ngassa alijifua kwa jumla ya saa mbili katika mazoezi hayo ya kwanza ambapo mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Brandts alimsifia nyota huyo huku akimtaka sasa kuthibitisha kuwa Yanga haikukosea kumsajili katika kikosi hicho.

“Namjua Ngassa, nilimuona wakati uliopita akiwa Simba, nimefurahi kumuona akiwa hapa tena katika siku ya kwanza, ameonyesha kujituma katika mazoezi ya leo.

“Lakini sasa anatakiwa kuthibitisha juu ya ubora wake akiwa na Yanga, nafahamu kuwa ana spidi na mbinu nyingi, nafikiri sasa anatakiwa kuonyesha hayo hapa,” alisema Brandts.


Kwa hisani ya Khatimu Naheka/ GPL

0 maoni: