Tuesday, 25 June 2013

Mwanawe Museveni asema hana uchu wa madaraka

Brigedia Muhoozi Kainerugaba, (wa pili kulia ) akiwa na babake rais Museveni wakati wa sherehe ya kufuzu kwake katika chuo cha mafunzo ya kijeshi nchini Marekani.
Mwanawe rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekanusha madai kuwa kuna mipango ya kutaka kumrithi babake huku akileta mwanga kwa madai ya upinzani kuwa anaandaliwa kuchukua madaraka baada ya babake kuondoka mamlakani mwishoni mwa utawala wake. "Uganda sio ufalme ambapo uongozi unarithiwa kutoka baba hadi kwa mwanawe, alisema Muhoozi Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 39, ambaye ni kamanda wa kikosi maalum cha jeshi nchini humo.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mtandao Jumapili usiku kulingana na gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda.
Mwezi jana polisi walifunga magazeti mawili ya binafsi nchini Uganda na vituo viwili vya redio kwa siku kumi baada ya kuchapisha barua kuhusu mgawanyiko jeshini kuhusiana na mpango wa rais Museveni kutaka kumkabidhi mwanawe mamlaka.
"uamuzi wa kuamua ambavyo Uganda itaongozwa ni jukumu la wananchi wenyewe wala sio mtu mmoja kama wanavyosema baadhi ya watu,'' inukuu taarifa ya Kainerugaba na ambayo ilitolewa na msemaji wa kikosi maalum cha jeshi la nchi hiyo, Edson Kwesiga.
Magazeti ya Daily Monitor na Red Paper yalichapisha barua iliyofichuliwa na ambayo ilikuwa na maudhui ya mpango wa kumrithisha mamlaka mwanawe Museveni. Barua hiyo iliandikwa na generali mkuu katika jeshi, David Sejusa, akidai kuwa Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1986 anamuandaa mwanawe kumrithi.
Sejusa, kwa jina lengine Tinyefuza, amekimbilia nchini Uingereza baada ya kudai kuwepo mpango wa kuwaua wanajeshi wanaopinga mpango huo, ingawa madai hayo yalikosolewa na majenerali wengine jeshini.
Kainerugaba, ambaye ni Brigedia, na ambaye anaongoza kikosi maalum cha jeshi, amekuwa akipandishwa cheo jeshini, ingawa rais Museveni hajatamka lolote kuhusu mpango wa kumkabidhi mamlaka mwanawe.
Kwesiga alisema kuwa mwanawe Museveni alitoa taarifa hiyo ili kueleza msimamo wake kuhusiana na madai hayo, kuwa wanamuandaa kuwa rais
Uganda inapaswa kuandaa uchaguzi mwaka 2016 lakini haijulikani ikiwa Museveni ambaye mwenyewe ni generali wa jeshi anapanga kuwania kwa mara nyingine.
Kwa hisani ya BBC Swahili

0 maoni: