Ilikuwa Juni 18, mwaka huu katika Uwanja wa Soweto wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikukusanyika ili kuwaaga watu wanne waliokufa kufuatia bomu lililolipuka Juni 15, katika uwanja huo. Tangu bomu hilo lilipolipuka siku hiyo (Jumamosi), viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe walifanya mikutano uwanjani hapo Juni 17 na 18, Japo tayari polisi walishazungusha utepe katika eneo lililolipukia bomu.
Siku hiyo, saa 9 alasiri wakati mkutano ukiendelea na viongozi wa chama hicho wakitoa maelekezo ya jinsi ya kuaga maiti, polisi waliokuwa wamefurika eneo hilo waliwashambulia kwa mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya. Malisa anayeishi Kata ya Ngarenaro jijini humo alifika uwanjani hapo kumwokoa baba yake Godwin Malisa ambaye ni mlemavu, alijikuta akipata kipigo cha mbwa mwizi.
“Nilikuwa namfuata baba yangu ambaye ni kada wa Chadema. Kutokana na ulemavu wake nilihofu angepata matatizo kama vurugu zingezuka,” anasema Wema na kuongeza:
“Nilikuta uwanja ukiwa umefurika wananchi wakiwasikiliza viongozi wa Chadema. Viongozi hao ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alihutubia na kumwachia Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) naye akamwachia Said Arfi (Mbunge Mpanda Kati). Alipomaliza kuwataka wanachama hao waelekee Hospitali ya Mount Meru, ndipo mabomu yakaanza kulipuliwa.”
Anaendelea kusema: “Nilimwambia baba tuondoke lakini tulikuwa tumeshachelewa, kwani polisi walikuwa wametuzingira. bomu la pili liliangukia mbele yetu. Askari mmoja akasema ‘laleni chini’, tukalala tukidhani tutakuwa salama. Lakini walikuja askari na kutupiga marungu mwili mzima mimi na baba,”
“Ghafla akatokea askari mwingine akawakataza wasitupige, tukadhani tumeokoka. Mara wakatokea askari wengine, hapo ndipo kilikuwa kipigo kitakatifu. Nilijaribu kuwazuia wasimpige baba kwa kuwa ni mlemavu, wakanikebehi kuwa huyo ni hawara yangu. Walinipiga mpaka mkono na mguu ya kushoto ikavunjika.
“Tulikuwa kwenye kibaraza cha nyumba wakati askari wanatupiga. Askari mmoja alirarua gauni langu chini na juu, hadi nikabaki uchi mbele ya baba. Mwingine akakoki bunduki na kuielekeza katikati ya mapaja yangu ili alipue sehemu za siri, wenzake wakamkataza. Mwingine alisema kuwa atanibaka. Baba alinikumbatia akasema watuue wote, mimi niliomba wasituue maana nimeacha mtoto mchanga nyumbani.”
Anasema askari walikuwa wakimbeza kwa kumuuliza kwa nini yeye ni mwanachama wa Chadema.
“Walisema ‘unajifanya wewe Chadema, sasa ndiyo utajua kuwa CCM inatawala. Chezea CCM wewe.’ Mimi niliwaambia sina chama chochote nimekuja kumwokoa baba yangu. Wakati huo wote walishanivua hereni, simu wakachukua na fedha zilizokuwa ndani ya pochi na kuitupa chini ikiwa tupu.”
Hata hivyo Wema anasema alikuja askari wa kike aliyekuwa akipiga picha za matukio na kuwasaidia. Wakati huo watu wote wameshatawanyika uwanjani hapo na askari wameshaanza kujipanga baada ya kuitwa kwa filimbi.
“Alitusikitikia na kusema, ‘kwa nini mnang’ang’ania kuwa Chadema? Angalieni sasa mlivyoumia na viongozi wenu wamewakimbia.’ Akaokota kanga iliyoachwa uwanjani na kuja kunifunika,” anasema na kuongeza:
“Kisha likaja gari la polisi tukabebwa na kuingizwa humo. Mwendo tuliondoka pale ulikuwa wa kasi huku wakiendelea kulipua mabomu na kutukanyaga bila kujali. Tulishtukia tuko Hospitali ya Mount Meru, tukabwagwa hapo na gari hilo likaondoka.”
Wema anasema walitibiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa ili kuugulia nyumbani.
Maelezo ya baba yake
Baba yake Wema, Godwin Malisa japo hakupata majeraha makubwa, anaendelea kuugulia maumivu makali ya mwili mzima.
“Kilichonisikitisha ni kitendo cha kumpiga na kumdhalilisha mwanangu mbele yangu. Askari wengine walikuwa wakijaribu kuvunja hili gongo ninalotembelea kwa sababu ya ulemavu,” anasema Malisa na kuongeza:
Alalamikia kauli ya Pinda
“Nimesikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa hivi karibuni Bungeni Dodoma ya kuwataka askari waendelee kupiga wananchi. Kwa hali hii sisi wanyonge natuna pa kukimbilia.”
Akisimulia zaidi, Malisa anasema, siku hiyo licha ya watu kuwa wengi katika uwanja huo, Jeshi la Polisi halikufuata kanuni zake za kutoa ilani kwa wananchi kabla ya kuanza kushambulia.
Licha ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha kusema hakukuwa na majeruhi siku hiyo, inaelezwa kuwa wengi walijeruhiwa kwa kupigwa na polisi.
Kauli ya Serikali
Akijibu maswali ya wabunge hivi karibuni bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu Mizengo amewahimiza polisi kuendelea kuwapiga wananchi wanaokiuka sheria, kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria.
“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki wewe ukakaidi, utapigwa tu...Maana hakuna namna nyingine. Maana lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria. Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba wewe ni imara zaidi, ni jeuri, watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna nyingine eh… maana tumechoka sasa.”
Habari na Elias Msuya, Arusha , Chanzo - Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment