Wednesday, 12 June 2013

Kifo cha KASHI... yametimia

KIFO cha msanii wa siku nyingi  katika tasnia ya filamu za Kibongo, Jaji Hamisi ‘Kashi’ kilichotokea Jumatatu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kimehitimisha maono ya mchungaji aliyetabiri kuwa mastaa wawili mmoja wa Bongo Fleva na mwingine wa Bongo Movie watafariki dunia ndani ya mwaka huu.


TAARIFA ZA KIFO

Saa 5 asubuhi taarifa za kifo zilitua katika chumba chetu cha habari na haraka waandishi wetu wakafika nyumbani kwa baba mzazi wa msanii huyo Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es Salaam na kuwashuhudia waombolezaji wakiangua vilio kufuatia kifo cha mpendwa wao huyo. Akizungumza na paparazi wetu rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mwamtoro Mzura alisema wiki mbili kabla ya kifo hicho, Kashi akiwa anaendesha gari maeneo ya Karume, Ilala jijini Dar alikosea njia na kwenda kujikita kwenye ukingo wa barabara na kuumia miguu.

“Baada ya kupata ajali hiyo alikimbizwa Hospitali ya Amana na kupatiwa matibabu, kisha akaruhusiwa kurudi nyumbani, kuanzia siku hiyo hali yake ilianza kudhoofu,” alisema. Mwamtoro alisema kuwa Ijumaa iliyopita hali yake ilibadilika na kuwa mbaya, hivyo akakimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu hadi Jumatatu iliyopita alipoaga dunia.



MASTAA WAFURIKA NYUMBANI KWAKE

Jacqueline Pentzel ‘Jack wa Chuz’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Mayasa Mrisho ‘Maya’, Seif Mbembe, Herieth Chumila, Happy Nyatawa ambaye alikuwa na marehemu katika Kundi la Shirikisho la Msanii Afrika. Mastaa hao walinaswa na mapaparazi wetu nyumbani kwa baba mzazi wa Kashi. Wengi wa mastaa hao walionekana kuangua vilio kwa nguvu kutokana na uchungu wa kuondokewa na mwenzao ambaye walikuwa wakishirikiana naye katika kazi zao za usanii wa filamu na mambo mengine ya kijamii.
WASANII WALIA NA MCHUNGAJI
Baada ya taarifa za msiba huo kusambaa, baadhi ya wasanii walipiga simu katika chumba chetu cha habari na kuuliza habari za mchungaji aliyetabiri kifo cha  msanii wa Bongo Fleva na wa Bongo Movie. “Kaka hivi yule mchungaji mliyemwandika katika gazeti ni nani na anapatikana wapi?” alihoji msanii mmoja mkubwa katika tasnia ya filamu za Kibongo. Kama vile haitoshi, simu nyingine za wasanii wa filamu zilimiminika katika chumba chetu cha habari kadiri wasanii hao walivyokuwa wakipata taarifa za msiba huo. Wasani hao wote walikuwa wakitaka kumjua mchungaji aliyetoa maono yake katika gazeti la Ijumaa la Machi 22-28, mwaka huu.



KUHUSU MCHUNGAJI

Kuhusu mchungaji ambaye alikataa katakata kutajwa jina lake gazetini alitoa wasifu wa wasanii watakaofariki dunia na kusema kuwa msanii wa kiume atakuwa ni wa Bongo Fleva na wa Bongo Movie ni wa jinsi ya kike.

MSANII WA BONGO FLEVA
Mchungaji alisema msanii wa Bongo Fleva si  mkongwe katika fani lakini anajulikana sana na ana mashabiki wengi. Nyimbo zake zinapendwapendwa na zinapigwa redioni na kuoneshwa kwenye televisheni (runinga) ambaye moja kwa moja wasifu huu unaangukia kwa Albert Mangwea ‘Ngwair’ aliyefariki dunia Afrika ya Kusini Mei 28, mwaka huu.

MSANII WA KIKE
Kwa mujibu wa mchungaji huyo msanii wa kike atakayefariki ni mkongwe kidogo halafu ni mweusi ambaye zamani aliwahi kuwika sana lakini kwa siku za hivi karibuni kidogo amepoapoa. Ukiangalia kwa undani wasifu huu utaona moja kwa moja unafanana na wa Kashi kuanzia rangi na jinsi alivyowika sana zamani na hadi kifo kinamkuta akiwa ameshapoapoa. 

MAZISHI
Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, habari zilizopatikana zilisema kwamba Kashi alikuwa akitarajiwa kuzikwa jana katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar.

WASIFU WAKE KIDOGO
Kashi alizaliwa mwaka 1978 mkoani Lindi, ameshiriki katika filamu mbalimbali ikiwemo ya Revenge akishirikiana na Vincent Kigosi ‘Ray’ pamoja na Blandina Chagula ‘Johari’.
Filamu nyingine zilizompa chati ni Out Of Mind, Mapito na Ukiwa. Msanii huyo ameacha watoto wawili wa kiume Muniri ambaye amemaliza kidato cha nne na mwingine wa kike aitwaye Fatuma anayesoma kidato cha nne.

NENO LA MCHUNGAJI
Baada ya kifo hicho cha Kashi, Risasi Mchanganyiko liliwasiliana na Mchungaji huyo ambapo alisema hivi karibuni atatoa utabiri mwingine ambao ni mkubwa kuliko uliopita. 
Mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi, amina.


Angalia picha za mazishi yake hapa chini






Habari na Gladdness Mallya na Richard Bukos wa GPL - Picha - Mpekuzi

0 maoni: