Monday 4 February 2013

Miss Tanzania ndani ya penzi la MUME wa mtu?

MREMBO ambaye mwaka jana aliiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya Urembo ya Dunia ‘Miss World 2012’ yaliyofanyika nchini China, amenaswa na mwanaume aitwaye Abed Zagar anayedaiwa ni mume wa mtu, Ijumaa Wikienda limenyetishiwa.Kunaswa kwa wawili hao kumekuja kufuatia picha zao ‘romantic’ zinazowaonesha wakila bata maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuvuja huku maelezo ya awali yakidai ni wapenzi na hilo halina kificho.

Chanzo chaanika
Awali, chanzo chetu kilichoomba hifadhi ya jina lake kilidai kuwa, Abed ana mke wake aitwaye Nasra lakini baada ya kukutana na Lisa ‘amekufa na kuoza’ kwake hivyo kujikuta akiwekeza penzi lake.

“Kwa kifupi Abed ana mke wake lakini nashangaa kuona anatoka na Lisa huyu Miss Tanzania wa mwaka jana, jaribuni kufuatilia lakini kiukweli Lisa anakosea kuinyevua ndoa ya mwenzake,” kilidai chanzo hicho ambacho ni mtu wa karibu wa Nasra na kuongeza: “Tuliona picha Lisa na Abed wakiwa wote China kwenye mashindano ya Miss World, tukahisi ni kampani ya kawaida tu lakini tumeshangaa kusikia ni wapenzi, kwa kweli inasikitisha.” Mwandishi wetu alimuomba ‘sosi’ huyo amuibue Nasra ambaye inadaiwa kwa sasa anaishi Uingereza ili afungukie sakata hilo lakini inavyoonekana mwanamke huyo anaogopa magazeti kama ukoma.

Abed asakwa
Baada ya kupata madai hayo, waandishi wetu walianza kumsaka Abed kupitia simu yake ya mkononi ambapo siku ya kwanza hakupokea na hata alipotumiwa meseji na kutakiwa kupokea simu ili asomewe madai hayo, hakujibu chochote licha ya sms kuonesha ‘delivered’. Siku ya pili alipopigiwa tena hakupokea lakini siku ya tatu (Ijumaa iliyopita) majira ya saa 7 mchana, mwandishi alikuta ‘missed call’ ya Abed na alipopigiwa na kutakiwa kufungukia madai hayo alisema, yeye si mpenzi wa Lisa na kama kuna picha zinazowaonesha wako pamoja, hiyo haimaanishi wanatoka.

Lisa afichua siri
Katika hali ya kushangaza, kabla Abed hajamaliza kuzungumza, Lisa ambaye pia ni Miss Tanzania namba 3, 2006 alimpokonya simu (inaonekana walikuwa pamoja) na kufichua siri nzito. Lisa alisema, anachojua yeye Abed ni mchumba wake na si mume wa mtu licha ya kwamba huko nyuma anajua alishawahi kuwa na wanawake wengine. “Abed ni mchumba wangu na ukweli ni kwamba mimi nafahamika kwao na yeye anafahamika kwetu kwa hiyo si jambo la siri, ndiyo maana nashangaa hayo madai kuwa eti ni mume wa mtu,” alisema Lisa, maelezo yanayoibua hisia tofauti kufuatia awali Abed kukana kutokuwa na uhusiano naye.


Angalia picha zaidi za Lisa na Abed hapa chini

0 maoni: